Polisi Tanzania yawaonya tena wanaopanga maandamano

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania, limewaonya kwa mara nyingine watu wanaopanga maandamano ya amani yasiyokuwa na kikomo, yaliyopigwa marufuku baada ya kukosa sifa za kisheria kufanyika kwa mujibu wa Katiba.

Maandamano hayo yaliyopangwa kuanza kufanyika jana Jumanne Desemba 9,2025 katika maeneo mbalimbali nchini, lakini yalishindikana baada ya polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene jana aliwashukuru Watanzania kwa kuonyesha utulivu na uzalendo katika kuilinda amani ya Tanzania, wakati Taifa likiadhimisha miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika.

Kwa mujibu wa polisi, baada ya maandamano hayo yasiyokuwa na kikomo kukwama jana Jumanne Desemba 9,2025 inadaiwa watu hao wamepanga kuyafanya leo Jumatano Desemba 10,2025.

Kabla ya kufikia uamuzi wa kuyapiga marafuku maandamano hayo Desemba 5, polisi ilianisha mambo 12 ikidai kuhamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani yaliyokuwa yakiendelea kupangwa mitandaoni kuelekea Desemba 9, huku likitoa onyo la kuwashughulikia watakaoandamana.

Leo Jumatano Desemba 10, 2025 akitoa taarifa ya mwenendo wa hali ulinzi na usalama, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime ametoa onyo kwa watu wanaopanga kufanya kile walichokiita maandamano yasiyokuwa na kikomo yaliyopigwa marufuku Desemba 5.

“Tumekuwa tukiwafuatilia kwa ukaribu na kwa muda mrefu toka jana (Desemba 9) kwenye hizo za mitandaoni na njia nyingine walizokuwa wanazitumia kuwasiliana, kupanga na kuhamasishana,” amesema.

“Kwa vile jana (Desemba 9) walishindwa kufanya maandamano hayo yaliyo kinyume na Katiba ya nchi ya mwaka 1977 na Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi wajitokeze mitaani leo Desemba 10,2025 kufanya maandamano hayo haramu,” amesema  Misime katika taarifa hiyo.

Misime amesema jeshi hilo, likishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, linawahakikishia wananchi litaendelea kulinda usalama wa nchi, sambamba na maisha na mali zao ili kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Misime amefafanua kama mtu atajitokeza na kukaidi kutii sheria za nchi kwa lengo la kuhatarisha usalama wa nchi, ili kusimamisha shughuli za kiuchumi na kijamii, kama wanavyohamasishana na kujidanganya watadhibitiwa katika kuhakikisha Taifa linabaki salama na Watanzania wanabaki salama.

“Tungependa kutoa wito kwa wananchi kuendelea kufanya shughuli zao na kufuata maelekezo watakayokuwa wakipewa na vyombo vya ulinzi na usalama maeneo yote nchini, sambamba na kutii sheria za nchi,” amesema Misime.