Waafrika tumepokea tamaduni za nje kwa namna mbalimbali. Wakati wa utumwa hali ilikuwa mbaya zaidi kwa sababu hakukuwa na namna. Watu walilazimishwa kukubali au kuuawa. Afadhali kidogo wakati wa ukoloni ambapo aliyekubali kubadilika alichukuliwa kuwa bora zaidi ya yule aliyebisha. Namna zingine zilizoathiri utamaduni wetu ni biashara na utandawazi. Lakini hizi zilikuwa na hiyari ya kuufuata utamaduni uupendao.
Utamaduni huambatana na mavazi, chakula, ngoma, hadithi na kadhalika. Hadithi ndiyo ilikuwa njia rahisi zaidi kwa sababu iliwafikia wengi bila gharama na katika kipindi kifupi. Moja ya hadithi hizi ni ile ya “Jini ndani ya chupa” iliyokuwa toka kwa Waarabu. Tumewasikia Wamarekani, Wahindu, Wachina na Waafrika wakiisimulia hadithi hii kwa njia tofauti ikiwemo kuucheza kwenye muziki wao.
Hadithi ilimwelezea jini aliyemkosea bwana wake. Akaadhibiwa kwa kuingizwa kwenye chupa na kutoswa baharini. Kwa bahati yake nzuri, jioni moja mvuvi alikwenda kutupa ndoano baharini humo kwa lengo la kuvua samaki. Ndoano ikaunasa mfuniko wa chupa. Kwa kuhisi kuwa amepata samaki mvuvi aliivua hiyo chupa na kuifungua. Ndipo alipotoka jini mkubwa aliyekuwa na hasira ya kuwekwa kifungoni kwa miaka yote hiyo.
Mvuvi kwa kulilia uhai wake akaomba shauri lao likasikilizwe na wazee wa pwani. Jini alikubali kwa sharti la kukubaliana na hukumu itakayomwondolea gadhabu zake. Kwa bahati nzuri mzee waliyemkuta pwani alishangazwa na umbo kubwa kama la jini kutosha kwenye chupa ya lita moja. Jini kwa kuondoa utata aliingia chupani na kusema “nilikaa hivi”. Papo hapo mzee aliifunga tena chpa ile na kumwamuru mvuvi akaitose kule alikoivua. Hiyo ndiyo ikawa salama ya mvuvi na wote waliomzunguka.
Hadithi hii inaonesha jinsi busara inavoweza kuamua mashauri hata yaliyo mazito kwa kiasi gani. Inawezekana mshangao wa yule mzee haukuwa halisi, bali ni busara zake zilizomwelekeza kupita njia hiyo ili kufika alipopataka. Ni kama mwamuzi wa kesi ingine ya mbwa mwitu dhidi ya binadamu. Mnyama huyu alinasa mtegoni, akamwomba binadamu amnasue. Aliponasuliwa na kuwa huru, mbwa mwitu akataka kumla binadamu.
Mwamuzi alikuwa mbweha. Naye alitumia njia kama hiyo kwa kujifanya kutokuelewa shtaka: “Yaani mtego ulikuwa unawinda, halafu binadamu akanasa…” Mbwa mwitu kwa hasira akasisitiza kwa vitendo: “Nasema huu mtego ulikuwa wazi kama hivi, mimi nilikuwa nawinda nikanasa hivi…” Mbwa mwitu alimalizia kwa kuingia mtegoni. Mbweha akaufunga na kumpa binadamu uhuru wa kuondoka zake.
Uzuri wa busara huwa haibishani. Yenyewe hutoka mwishoni baada ya kuchenjua kwa makini hoja za kila upande. Wakati wote busara hushinda kwa sababu haipendelei wala kudhulumu upande wowote. Hata kama ugumu wa shauri unakuwa mkubwa kwa kiasi gani, busara haijawahi kushindwa mahali popote. Kwenye vitabu vya kale tunasoma habari za akina Suleiman walioamua kesi ngumu kwa kutegemea busara.
Iwapo tunategemea busara kuendesha familia zetu, viongozi nao watumie busara zaidi kuendesha jamii. Baada ya yale yaliyotokea Oktoba 29, 2025 tunatarajia busara itumike zaidi ya amri. Watanzania ni watoto wa Tanzania, hivyo inafaa kwa mamlaka kufanya nao mashauri kama vile mzazi afanyavyo na mtoto wake. Mtoto apewe nafasi ya kulalamika, kushauri na hata kukemea anayoyaona hayapo sawa ndani ya familia.
Hivi ndiyo tunavyowalea watoto wetu wa leo. Na tutegemee kuwa watajiongeza kwa sababu wanaishi, kusoma na kucheza na wenzao tofauti. Katika majadiliano yao, wanaweza kung’amua namna bora ya kuendesha mambo yao. Wakati mwingine tunaowaona kama wanaokosea wanapofanya mambo kivyao. Kwa mfano wanapoketi pamoja na wazee, wakati mwingi wao huutumia kwenye simu.
Kumbe hiyo ndio njia yao ya kupashana kwa jumbe fupi (sms): “Unamwona dogo janja? Kishavesha (kalewa) sasa anatuchoresha kwa mabuda”. Na jibu linarudishwa: “Mtxt bigi amwondoe”. Tatizo linakuwa ni kutokuelewana tu; wakati vijana wanajitahidi kuidumisha heshima mbele ya wazee wao, wazee wanadhani wanadharaulika kwa watoto kuchezea simu badala ya kuwasikiliza.
Kumbe ni muhimu kwa wote kupaona pale ufa unapowagawanya. Kwa hekima za kibinadamu, zitafutwe njia zinazoweza kuwaunganisha tena wote wakaongea lugha inayoeleweka na wote. Naamini kwa kuwa wazee walishaupita ujana wananielewa vizuri kuliko vijana ambao hawajapata kuwa wazee. Mwenye busara husikiliza zaidi. Huzingatia kuwa ni bora kusikiliza zaidi ili kujenga kuliko kusema zaidi ili kubomoa.
Zamani tuliona maajabu kwa wazungu, pale baba aliposhauriana na mwanaye mambo nyeti ya kifamilia. Mara nyingi tuliona mtoto akimwita baba yake na kumwonya juu ya mwenendo wake kwenye familia. Kiafrika hakuna mtoto aliyethubutu kuwa na ujasiri huo; angekula mikwaju yeye na mama yake. Lakini hivi sasa Tanzania ni moja kati ya nchi zinazozingatia haki za rika na jinsia.
Ninaamini Tume iliyoundwa na Mheshimiwa Rais itaendesha maridhiano kwa usawa miongoni mwa makundi yote. Pia itatumia busara katika kuileta Tanzania pamoja tena, ibaki kuwa nchi ya kupigiwa mfano duniani kote kama mwanzo. Mwenyezi Mungu atuepushie mbali na mzimu uliopita. Yaliyopita yabaki kuwa hadithi tu ya kuvitahadharisha vizazi vyetu vinavyokuja. Amen.
