LHRC yataka Katiba mpya, uwajibikaji wa vyombo vya dola

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa wito wa kushughuliwa vikwazo dhidi ya haki za binadamu nchini na kuzingatiwa kwa mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo nchi imeridhia.

Katika taarifa yake ya maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani, leo Jumatano, Desemba 10, 2025, LHRC imeeleza changamoto za haki za binadamu nchini hasa kwa mwaka huu 2025 ambao Taifa lilifanyaΒ  uchaguzi wake mkuu.

Desemba 10, kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Haki za Binadamu katika kutambua na kuhamasisha juhudi za ulinzi wa haki za binadamu, kama ilivyoainishwa katika Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu (UDHR) lililopitishwa na Umoja wa Mataifa, Desemba 10, 1948.

Taarifa hiyo imeeleza mambo kadhaa yakiwamo matukio ya ukamataji wa watu wenye maoni kinzani, utekaji na upoteaji wa watu, mauaji ya raia, kufunguliwa mashitaka ya uhaini kwa wakosoaji wa SerikaliΒ  pamoja na kuzimwa kwa huduma za mitandao ya kijamii na intanetiΒ  Oktoba 29, 2025 katika uchaguzi mkuu kuwa, yanakiuka haki za binadamu.

Katika wito wake kwa Serikali, LHRC imeiasa kuzingatia na kuendelea kuridhia mikataba ya kimataifa na kikanda, kuanzisha mchakato wa Katiba mpya, kuachilia huru waliokamatwa kinyume cha sheria na kuwawajibisha watendaji wa vyombo vya dola wanaohusika na uvunjifu wa haki za binadamu.

LHRC pia, imetoa wito kwa Serikali kulinda uhuru wa kuabudu, uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa wanahabari sambamba na uhuru wa kujieleza.

“Licha ya Tanzania kuorodheshwa na Chandler Good Government Index 2025 kama moja ya nchi zilizopiga hatua katika utawala bora na maridhiano ya kisiasa, imekumbwa na changamoto kadhaa hususan kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba,” imeeleza taarifa hiyo.Β 

LHRC imetaja matukio kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari na kukamatwa kwa wanahabari kuwa ni baadhi ya vikwazo katika haki za binadamu nchini.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, zaidi ya watu 2,045 walikamatwa wakati na baada ya uchaguzi huku takribani 900 wakifunguliwa mashitaka mbalimbali ikiwamo uhaini na ujambazi wa kutumia silaha.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali kwa nyakati tofauti wamethibitisha kukamatwaΒ  na kuachiwa kwa baadhi ya watuhumiwa wa vurugu za maandamano ya Oktoba 29, 2025 huku wakisisitiza dhamira ya kulinda usalama wa raia na kuimarisha maridhiano ya kisiasa.Β 

Taarifa hiyo ya LHRC pia imeeleza kuhusu kuzimwa kwa mitandao ya kijamii ikiwamo X (zamani Twitter), TikTok na JamiiForums, jambo lililotajwa kuathiri upatikanaji wa taarifa kwa wananchi.

Hata hivyo, Serikali imeendelea kutumia mitandao ya kijamii kuwasiliana na umma kwa taarifa zake mbalimbali huku ikisisitiza kuwa, hatua zake za kudhibiti maudhui mitandao zinalenga kudumisha utulivu na usalama wa Taifa.Β 

Katika upande wa uhuru wa kuabudu, LHRC imetaja changamoto kadhaa ikiwamo kufungiwa kwa baadhi ya taasisi za kidini na malalamiko ya viongozi wa dini, huku Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikisisitiza kulindwa kwa haki hiyo.

Taarifa hiyo ya LHRC imekuja wakati Serikali ikichukua hatua mbalimbali katika kubaliana na matukio yanayochochea uvunjifu wa amani ikiwamo kudhibiti maandamano yanayoratibiwa mitandaoni na watu wanaofaiwa kuwa ni wanaharakati na vijana (Gen Z).

Aidha, Serikali imeendelea kusisitiza dhamira ya kulinda haki za binadamu, amani na utulivu nchini tangu kutokea kwa vurugu za uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 zilizosababisha vifo vya watu ambao idadi yao haijawekwa wazi na uharibifu wa mali za umma na watu binafsi.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wazee wa Dar es Salaam, jijini Dar es Salaam hivi karibuni alisisitiza kuwa, Serikali itaendelea kulinda amani ya nchi kwa nguvu zote kulingana na ukubwa wa maovu yatakayokuwa yakipangwa au kutokea.

Tayari Rais Samia alishaunda tume ya kuchunguza kilichotokea katika vurugu hizo kwa lengo la kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Pia, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam,Β  Novemba 25, 2025, alikiri kuwa vurugu zilizotokea katika uchaguzi huo zilisababisha madhara makubwa kwa Taifa.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kuhakikisha matukio kama hayo hayatokei tena.

Β β€œSerikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha usalama wa raia na kuimarisha mshikamano wa kitaifa,” alisema.

Kwa upande wa utawala bora, Ripoti ya Chandler Good Government Index 2025 iliyotolewa Septemba 8, 2025 iliorodhesha Tanzania katika nafasi ya 78 duniani kati ya nchi 120, ikiwa ndiyo nchi iliyopiga hatua kubwa zaidi barani Afrika.

Katika ripoti hiyo ya utawala bora duniani, Tanzania ilipanda kutoka nafasi ya 98 mwaka 2024 hadi 78 mwaka 2025, ikitajwa kuwa na maboresho katika uongozi, mageuzi ya kidijitali na uwekezaji ni miongoni mwa vigezo vilivyoipaisha Tanzania.

Hata hivyo, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa, hatua zinazochukuliwa zinajikita kulinda usalama wa Taifa na kuimarisha maridhiano ya kisiasa.

Sambamba na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa, Serikali imekuwa ikisisitiza kulinda uhuru na mamlaka ya nchi kwa kukataa kuongozwa kwa maelekezo na matamko ya mataifa ya nje katika kuamua mambo yake ya ndani.

Aidha, Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa, Tume ya Uchunguzi wa matukio ya Oktoba 2025 iliyoundwa na Rais Samia itasaidia kutambua na kumaliza tofauti za kisiasa zilizopo nchini na kuwezesha kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya