Irene anayekabiliwa na kesi ya uhaini, aongezewa kesi nyingine

Dar es asalaam. Mkazi wa Wazo Zahanati eneo la Tegeta, Irene Mabeche(58) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka moja la kuhamasisha umma kufanya vitendo vya uhalifu na kufanya maandamano katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.

Irene, ambaye ni mjasiriamali, anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu 340 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Mshtakiwa huyo ambaye pia anakabiliwa na kesi nyingine ya uhaini katika mahakama hiyo, amepandishwa kizimbani leo Jumatano, Desemba 10, 2025 na kusomewa shtaka lake na wakili wa Serikali, Eric Davies.

Wakili Davies ameieleza Mahakama kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 28914 ya mwaka 2025 yenye shtaka moja la kuhamasisha umma kufanya vitendo vya uhalifu na maandamano.

Davies ametoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki na kisha kumsomea mashtaka yake.

Mshtakiwa, Irene Mabeche (58) akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne Desemba 10, 2025. Picha na Hadija Jumanne.

Katika kesi hiyo, Wakili amedai kuwa mshtakiwa anadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2025 na Oktoba 29, 2025 katika eneo la Tegeta, Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam mshtakiwa kwa makusudi alishawishi umma kutenda makosa ya kihalifu ambayo ni kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria na kuhamasisha watu kuandamana na kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29, 2025 usifanyike.

Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka lake, alikana kuhusika na tuhuma hizo.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi umekamilika hivyo wanaomba mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya hatua nyingine.

“Kesi hii ilipangwa kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube, ambaye leo tumeambiwa amepata udhuru, hivyo kutokana na hali hii tunaomba mahakama itupangie terehe nyingine kwa kutajwa na siku hiyo hakimu husika atatupa utaratibu” amedai Davies.

Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa Jamhuri, ametoa masharti ya dhamana kwa kuwa shtaka linalomkabili mshtakiwa huyo linadhaminika.

Hakimu Nyaki amesema mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wanaotambuliwa kisheria watakao saini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.

Hata hivyo, mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Vile vile , kesi ya uhaini inayomkabili mshtakiwa huyo haina dhamana, hivyo anaendelea kusalia  mahabusu hadi Desemba 16, 2025 itakapotajwa kesi yake.

Hii ni mara ya pili kwa mshtakiwa huyo kufikishwa mahakamani hapo na kusomewa kesi mbili tofauti.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Novemba 7, 2025 na wenzake 94 na kusomewa kesi ya uhaini, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.

Kesi hiyo ya uchunguzi wa awali(PI) namba 26387 ya mwaka 2025 ilikuwa na mashtaka mawili, ambayo ni kula njama na kutenda kosa la uhaini.