Mawaziri wanne watua Pwani, wapewa kero nne

Pwani. Wawekezaji katika Kongani ya Viwanda Kwala, Mkoa wa Pwani, wamepaza sauti wakitaka kupatiwa umeme wa uhakika, maji, kuwekewa kituo cha treni ya umeme (SGR), na nafuu za kikodi walizoahidiwa mwanzoni.

Wametoa changamoto hizo leo, Jumatano, Desemba 10, 2025, walipotembelewa na mawaziri wanne wa kisekta na Serikali imewahakikishia kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.

Mawaziri hao na wizara zao kwenye mabano ni Profesa Kitila Mkumbo (Mipango na Uwekezaji), Judith Kapinga (Viwanda na Biashara), Jumaa Aweso (Maji), na Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba.

Akizungumza mbele ya mawaziri hao, Mwenyekiti wa Kongani ya Viwanda ya Kwala, Janson Huang, ametaka suala la umeme, maji, kuwepo kwa kituo cha treni ya umeme, na vivutio vya kodi walivyopewa awali kushughulikiwa.

Amesema kushughulikiwa kwa changamoto hizo kutaweka urahisi wa manufaa ya uwepo wa kongani hiyo kuonekana, kwani wataweza kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa baada ya kufanya uwekezaji kusudiwa.

“Tunahitaji umeme wa uhakika, maji ya uhakika, na pia tunahitaji miundombinu kamili ya kufikia eneo hili la viwanda, tunahitaji kituo cha abiria, sehemu ya bandari kavu kwa ajili ya kuhudumia viwanda, na vituo vingine pamoja na huduma nyingine muhimu,” amesema.

Amesema licha ya Serikali kuendelea kutoa usaidizi mzuri, bado wanahitaji kazi zaidi ifanyike katika baadhi ya maeneo.

Ametolea mfano wa mahitaji ya umeme, akisema kiwanda kimoja pekee cha kuzalisha vifaa vya umeme jua kinahitaji megawati 50, huku mahitaji ya maji yakiwa mita za ujazo 5,000 kwa siku.

“Hii ni kampuni moja tu. Tuna kampuni nyingi na viwanda vingi vinavyozidi kuja, kwa hiyo tunahitaji sana msaada wa miundombinu.

“Lakini tunafurahi kwamba leo, mawaziri wametuhakikishia changamoto zetu kwa vipindi tofauti ikiwemo umeme, maji, reli, miundombinu ya bandari kavu, na mambo mengine yatatatuliwa. Kwa hiyo tunafurahi, na tunaamini kwamba Tanzania ni moja ya maeneo bora barani Afrika katika mazingira ya biashara na viwanda. Tanzania pia ni sehemu bora kwa uwekezaji wa China,” amesema.

Kongani hiyo ya viwanda, itakapokamilika, inatarajiwa kutoa ajira 100,000 za moja kwa moja na ajira 500,000 zisizo za moja kwa moja.

“Tunashukuru kwa msaada wa Serikali ya Tanzania, na sisi pia tumejipanga kuhakikisha kongani hii ya viwanda inakuwa moja ya kongani bora zaidi barani Afrika,” amesema.

Akieleza kile kinachofanyika kushughulikia changamoto hizo, Profesa Kitila amesema suala la umeme na maji litatekelezwa kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta Binafsi na Serikali (PPP).

Amesema wanatambua ujenzi wa Tanzania ya viwanda hauwezekani bila nishati ya uhakika, hivyo suala hilo limebebwa kwa uzito.

“Watahitaji hadi megawati 100 kwa matumizi ya kawaida, lakini kwa kuanzia tumekubaliana kuwa wiki mbili zijazo watapata megawati nne, watawekewa transfoma kutoka Mlandizi,” amesema.

Baadaye, kupitia mradi wa ubia, utajengwa mradi utakaowezesha upatikanaji wa Kilovoti 220, na watalipia ujenzi wa mradi huo, kisha watapata mrejesho wa fedha kupitia mauzo ya umeme yatakayofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Kuhusu maji, Profesa Mkumbo amesema katika siku za usoni eneo hilo litahitaji hadi lita milioni 1.5, na mfumo wa PPP utatumika.

“Kwa sasa watapewa kisima, lakini baadaye kuna mradi wa Sh25 bilioni wa maji utakaojengwa eneo hili na watalipana baadaye kupitia mauzo yatakayofanyika,” amesema.

Kuhusu upatikanaji wa kituo cha treni ya SGR katika eneo la Kwala, amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maagizo hayo na yanafanyiwa kazi.

Mbali na ile iliyopo sasa, Kwala imeanza utengenezaji wa vifaa vya kuzalisha umeme kwa kutumia jua, kiwanda kinachotajwa kuwa kikubwa Afrika nzima.

“Tayari wameshapata soko nchini Marekani. Kiwanda hiki ni muhimu katika ujenzi wa uchumi wetu, si katika kutoa ajira pekee bali pia kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi,” amesema.

Kikiwa na uwekezaji wa Sh2 trilioni kitakapokamilika, mauzo yake ya nje yanatarajiwa kufikia Dola milioni 300 za Marekani kwa mwaka wa kwanza na mwaka wa pili yatafikia Dola milioni 600.

Pia uwekezaji unatarajiwa kufanyika katika kiwanda cha kuchakata chuma, jambo litakalofanya malighafi inayotoka kwenye mradi wa Liganga na Mchuchuma kupata thamani ya juu zaidi.

“Kwa kuanzia watawekeza Dola milioni 50 za Marekani, hii inafanya chuma kutoka Liganga na Mchuchuma kuwa na sehemu ya kuongeza thamani,” amesema.

Amesema lengo kuu la Dira 2050 ni kujenga uchumi jumuishi unaotegemea viwanda, huku mfumo wa matumizi ya kongani za viwanda ikiwa ndiyo njia inayotumiwa maeneo mengi.

Amesema hadi sasa Tanzania ina kongani 34 za viwanda zilizosajiliwa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Tiseza), na mojawapo ni Kwala, iliyopo mkoani Pwani.

Mpaka sasa zaidi ya Sh625 bilioni zimeshawekezwa katika eneo la Kwala, na pindi ujenzi wa viwanda vyote 200 utakapokamilika, thamani ya uwekezaji itakuwa zaidi ya Sh10 trilioni.