Malale, Baresi watajwa KMC | Mwanaspoti

UONGOZI wa kikosi cha KMC unaendelea na mchakato wa kusaka kocha mpya atakayerithi nafasi ya Mbrazil Marcio Maximo, huku Kocha, Malale Hamsini aliyeachana na Mbeya City hivi karibuni na Abdallah Mohamed ‘Baresi’ wakitajwa ndani ya timu hiyo.

Maximo aliachana na kikosi hicho Desemba 6, 2025, baada ya kudumu kwa siku 131, tangu alipotambulishwa, Julai 28, 2025, ambapo kwa msimu wa 2025-2026, aliiongoza KMC katika mechi tisa za Ligi Kuu, akishinda moja, sare moja na kuchapwa saba.

Mwenendo huo mbaya kwa kocha huyo ukaufanya uongozi kuvunja mkataba wake ambapo kwa sasa miongoni mwa makocha wanaotajwa ni Malale aliyeachana na Mbeya City, Novemba 30, 2025 na Baresi anayeifundisha timu ya Zimamoto ya visiwani Zanzibar.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC (CEO), Daniel Madenyeka, alisema kuna makocha wengi ambao wametuma maombi (CV) ya kukifundisha kikosi hicho, ingawa hadi sasa hakuna muafaka wa kocha aliyepitishwa moja kwa moja.

“Tuna orodha ya makocha wazawa na wageni wanaohitaji nafasi lakini hatujafikia uamuzi wa mwisho wa kupitisha jina moja kati ya yaliyopo, kuanzia wiki ijayo timu itakaporejea mazoezini mchakato huo utakuwa umekamilika,” alisema Madenyeka.

Malale alijiunga na Mbeya City Machi 31, 2025, akichukua nafasi ya Salum Mayanga aliyejiunga na Mashujaa, ambapo kocha huyo wa zamani wa maafande wa JKT Tanzania, kwa msimu wa 2025-2026, alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya mechi tisa.

Katika mechi hizo tisa ambazo Malale aliiongoza Mbeya City, ilishinda mbili, sare mbili na kuchapwa mitano, ambapo kwa ujumla kikosi hicho kilifunga mabao saba na kuruhusu 10, huku Malale akiiacha ikiwa katika nafasi ya 10 na pointi nane.

Kwa upande wa Baresi, mara ya mwisho kufundisha timu ya Ligi Kuu Bara, ilikuwa ni maafande wa Mashujaa, ambayo aliachana nayo Februari 26, 2025, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kikosi hicho kuchapwa mabao 3-0, dhidi ya Singida Black Stars.