Arusha. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimefungua kesi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) ikikilalamikia hatua ya Serikali ya kuzima mtandao kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 4, 2025.
Kesi hiyo namba 56/2025 imewasilishwa Desemba 3,2025 ikiomba mahakama itamke kuwa kuzimwa kwa huduma za intaneti ilikiuka vifungu 6(d), 7(2) na 8(1)(c) vya Mkataba wa EAC wa mwaka 1999.
Mbali na kutamka hivyo, pia LHRC inaiomba mahakama ya EACJ kutoa amri inayozuia Serikali kurudia tena kuzima mtandao bila sheria au amri halali ya mahakama.
Kesi hiyo inayowakilishwa na mawakili wa LHRC, Wakili Peter Majanjara na Wakili Jebra Kambole.
Majanjara amesema kuwa wamefikia hatua ya kufungua kesi hiyo kutokana na kuzimwa kwa mtandao ghafla saa tano asubuhi siku ya Oktoba 29 na kuathiri huduma zote za mawasiliano nchini kwa siku saba mfululizo.
Amesema kuwa hatua hiyo iliathiri Watanzania kiuchumi na kijamii, ikiwemo kukwama kwa miamala ya benki mtandaoni, huduma za afya za kimtandao, pamoja na kupotea kwa fursa muhimu za kupata taarifa katika kipindi cha uchaguzi.
“Kitendo hicho kilisababisha hasara ya mamilioni ya shilingi kwa Watanzania na wawekezaji nchini, ambao hutegemea intaneti kwa shughuli zao za kila siku,”amesema wakili huyo.
Amesema kuwa sababu kubwa Serikali iliyotoa ya kuzima mtandao ni kuzuia vurugu, lakini sisi tunaona sababu hiyo haikidhi misingi ya demokrasia, haikuwa ya kisheria, wala ya lazima.
Aidha baada ya kufunguliwa kwa kesi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali atajibu maombi hayo ndani ya siku 45 baada ya kupokea nakala kutoka kwa Msajili wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.
Oktoba 29 siku ya uchaguzi mkuu, Serikali ilizima huduma ya intaneti kwa siku sita baada ya vurugu za maandamano yaliyotikisa mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Songwe.
Akilizungumzia hilo, msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa alisema Serikali imefanya hivyo kuhakikisha kuwa inazuia wahalifu mtandaoni ambao walitumia mitandao kueneza habari za uchochezi na kusababisha maandamano ya vurugu zilizopelekea watu kadhaa kuuawa, kujeruhiwa na uharibifu wa mali za umma na binafsi.