Wagosi wa Kaya waitana kujadili ripoti ya kocha

MABOSI wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ wanatarajia kufanya kikao keshokutwa Jumatatu pamoja na kocha mkuu wa timu hiyo, Mohammed Muya kwa nia ya kujadili ripoti ya usajili unaotarajiwa kufunguliwa Januari mwakani.

Coastal kama timu nyingine za Ligi Kuu ipo mapumziko kupisha Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zinazotarajiwa kuanza Desemba 21 hadi Januari 18 mwakani, huku Tanzania ikiwa ni kati ya timu 24 shiriki katika fainali hizo zinazofanyikia Morocco.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Muya amesema ripoti ya usajili amekabidhi kwa viongozi ambao wamemuomba Jumatatu wakutane kwa ajili ya kuijadili ili wajue pakuanzia na kuifanyia kazi.

“Naanza safari ya kwenda Tanga, nimeitwa na viongozi hivyo kuhusu ni maeneo gani tutafanyia kazi dirisha lijalo majibu yatatokana na kikao hicho,”   amesema Muya na kuongeza;

“Timu bado inaendelea na mapumziko hiki ni kikao changu na viongozi nafikiri ni kujua mustakabali wa usajili na kikao hicho kitatoa picha ni namna gani tutaboresha kikosi chetu ambacho bado hakina muendelezo mzuri wa matokeo.”

Hata hivyo, Muya hakutaka kuweka wazi ripoti yake inahitaji maboresho nafasi gani akisema anaamini uongozi utafanyia kazi mapendekezo yake ili kujenga timu ya ushindani.