Hii hapa ratiba ya mgawo wa maji Dar

Dar es Salaam. Kutokana na uhaba wa maji jijini Dar es Salaam, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira  (Dawasa) imetangaza ratiba ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa mpango wa dharura kwa wakazi wa jiji hilo, hatua inayolenga kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa usawa wakati wa changamoto za uzalishaji na usambazaji.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa leo Jumamosi Desemba 13, 2025, mgawo wa maji umegawanywa kwa kanda mbalimbali zikiwamo Kimara, Mshikamano, Bangulo, Kisarawe pamoja na maeneo yanayohudumiwa na matanki makuu ya Kisanga, Salasala, Vikawe, Changanyikeni, Mbweni na Tegeta A.

Katika kanda ya Kimara hadi Mjini Kati, maji yatapatikana kwa siku ya Jumapili hadi Jumatano, yakihudumia maeneo ya Kimara, Ubungo, Kijitonyama, Mwenge, Muhimbili, Msasani, Masaki, Upanga na maeneo ya kati ya jiji.

Ratiba hiyo pia inaonyesha mgao kwa njia za Kimara–Tazara, Kimara–Magomeni na Kimara–Kibamba na Unyamwezini kwa siku ya Jumatatu.

Kwa upande wa kanda ya Mshikamano, mgao utahusisha maeneo ya Makabe, Mbezi Mwisho, Machimbo na Madafu/Takukuru, huku baadhi ya maeneo yakipata maji kwa siku mbili hadi tatu kwa wiki kulingana na njia ya usambazaji.

Ratiba hiyo pia imeainisha huduma kwa kanda ya Bangulo, ikijumuisha maeneo ya Segerea, Temeke, Kiwalani, Yombo, Buza na Kipawa, pamoja na maeneo ya Kisarawe yanayokwenda Ukonga, Pugu, Buyuni, Chanika na Chamanzi.

Dawasa imewataka wananchi kufuatilia ratiba hiyo na kuhifadhi maji pale yanapopatikana, huku ikiomba uvumilivu wakati mamlaka hiyo ikiendelea kuchukua hatua za kiufundi kurejesha hali ya kawaida ya uzalishaji na usambazaji wa maji.