Vigogo kushiriki ibada ya kuaga mwili wa Mhagama

Dodoma. Viongozi mbalimbali Serikali na wabunge wameanza kuwasili katika Kanisa Katoliki Kiwanja cha Ndege kwa ajili ya ibada ya mwisho ya kuaga mwili wa aliyekuwa mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama.

Ibada hiyo inatarajia kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba na viongozi wengine wa chama na Serikali.

Miongoni mwa waliokuwa wa kwanza kuwasili ni Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda aliyeongozana na mawaziri wa zamani, Profesa Joyce Ndalichako na Margaret Sitta.

Mhagama alifariki asubuhi ya juzi Desemba 11, 2025 ambapo taarifa zinaeleza kuwa aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake Itega jijini Dodoma.

Taarifa za kifo chake zilitangazwa na Spika wa Bunge, Mussa Zungu na kwamba leo Desemba 13, 2025, mara baada ya ibada, mwili wake utasafirishwa kwenda Songea mkoani Ruvuma ambako watafanya ibada ya kumuaga, kisha kuelekea Peramiho kwa wapigakura wake kabla ya mazishi yatakayofanyika Jumanne Desemba 16, 2025 wilayani Mbinga.

Ndani ya kanisa kunaonekana kuwa na maandalizi makubwa huku maeneo ya nje kukiwa na ulinzi mkali kuzunguka jengo la kanisa na maeneo jirani.

Awali, ratiba ilimtaja Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi kwamba angeongoza viongozi katika ibada hiyo, lakini baadaye ikatolewa taarifa kuwa Rais Samia atakuwepo.

Profesa Ndalichako ambaye amekuwa hataki kuzungumza ndiye alikuwa rafiki wa karibu zaidi na marehemu Jenista na mara kadhaa waliingia bungeni wakiwa wamevalia mavazi yenye kufanana.

Tangu msiba ulipotokea juzi, Profesa Ndalichako ameonekana eneo la msiba muda wote na mara nyingi akiwa na watoto wa marehemu na kila alipotakiwa kuzungumza jambo lolote alikuwa akifuta machozi.