TRA yapanua wigo wa kodi kuzuia magendo na ukwepaji kodi

Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amesema wamejipanga kuongeza wigo wa kodi kwa kuzuia ukwepaji kodi na magendo.

Amesema hayo Desemba 12, 2025, alipofanya mkutano na mawakala wa forodha na washauri wa kodi Jijini Dar es Salaam, ili kubaini changamoto wanazokabiliana nazo na kuzitafutia ufumbuzi.

Hili linaelezwa wakati ambapo kumekuwapo malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali wakiitaka TRA kutanua wigo wa kodi ili kuongeza kiwango cha mapato kinachokusanywa, hasa baada ya kundi kubwa linalotakiwa kulipa kodi kutofikiwa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenda amesema vitendo vya ukwepaji kodi vinapunguza ushindani wa biashara sokoni na imani ya walipakodi wazuri, hali ambayo inaendelea kupunguza wigo wa kodi.

“Tunajua upo ukwepaji kodi unaofanyika kwa namna mbalimbali, ikiwemo kufanya magendo, kutokutoa risiti za mauzo, kufanya makadirio ya uongo na njia nyingine nyingi ambazo mnazijua. Hivyo tunawaomba muisaidie nchi kwa kufichua ukwepaji kodi,” amesema Mwenda.

Mwenda amesema kila mmoja ana wajibu wa kulipa kodi na kuisaidia nchi kujitegemea kwa mapato, kwa kulipa kodi kwa wakati na kwa hiari.

Takwimu zilizotolewa na Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) jana zilionesha kuwa asilimia 80 ya kodi inakusanywa kutoka kwa walipakodi wakubwa 400, na asilimia inayobaki inapatikana kwa wengine.

Akizungumzia hesabu za mwisho wa mwaka 2025, amewataka walipakodi nchini kutimiza wajibu wao, ikiwemo kuwasilisha ritani za kodi ya ongezeko la thamani kwa wakati, ili wamalize mwaka 2025 bila madeni ya kodi, hali itakayowaepushia riba na adhabu.

Mwenda amesema wameamua kufanya mkutano huo kwa sababu asilimia 75 ya makusanyo ya kodi nchini yanatokana na huduma za washauri wa kodi, ndiyo maana kulikuwa na umuhimu wa kukutana nao ili kubaini changamoto zinazojitokeza na kuweka mazingira yatakayoongeza imani ya walipa kodi.

Amesema TRA ina wajibu wa kuhakikisha ustahimilivu wa biashara, urahisishaji wa huduma, na kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki ili kupambana ipasavyo na ukwepaji kodi.

Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa), Edward Urio, ametoa wito kwa walipakodi kufuata sheria za kodi kwa kutimiza wajibu wao wa kukamilisha mwaka bila madeni ya kodi.

“Kwa upande wetu, mawakala wa forodha, majukumu yetu yamerahisishwa kupitia mfumo wa TANCIS ulioboreshwa, ambao umekuwa ukiturahisishia uondoshaji wa mizigo kutokana na kufanya taratibu zote kupitia mtandao,” amesema.

Naye mwakilishi wa washauri wa kodi, Victoria Soka, amesema wao kama washauri wa kodi watakwenda kutimiza wajibu wao kwa kuwashauri wateja wanaowahudumia watimize wajibu wao kwa wakati ili kuisaidia nchi kujitegemea.