Mwanza. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Mwadhama Protase Kadinali Rugambwa ameshauri vyuo vikuu nchini kuweka mwongozo wa matumizi ya Akili Mnemba (AI) ili kuepuka matumizi holela na ya kupitiliza kwa wanafunzi.
Amesisitiza kwamba matumizi ya AI yakikithiri, yatasababisha taifa kuzalisha wasomi wasio na uwezo wa kutafakari na kujenga hoja.
Rugambwa ameyasema hayo leo Jumamosi Desemba 13, 2025 wakati akizungumza katika mahafali ya 28 ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (Saut) kampasi kuu jijini Mwanza.
Katika hafla hiyo, Rugambwa amewatunuku shahada ya uzamivu (PhD), shahada ya uzamili, stashahada ya udhamiri, shahada ya kwanza, astashahada na stashahada, jumla ya wanafunzi 2,976 wakiwemo wanawake 1,543 sawa na asilimia 51.85 na wanaume 1,433 sawa na asilimia 48.15.
Amesema dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kasi ya sayansi na teknolojia ikiwemo matumizi ya AI ambayo imechukua nafasi ya wasomi kufanya tafakuri, kujenga hoja na kutoa suluhisho kwa changamoto zinazoikabili jamii.
“Ujio wa AI ambayo wakati mwingine taarifa zake siyo sahihi, je wasomi mnaisaidiaje jamii ili hii teknolojia isaidie jamii. Bahati mbaya AI imepenya mpaka kuta za vyuo vikuu,” amesema Rugambwa na kuongeza:
“Naiona hatari ya wasomi kukabidhi majukumu AI na wao kwenda likizo ya kutafakari. Vyuo vikuu vinatakiwa kuwa na mwongozo wa namba ya kutumia AI, itumieni AI kwa matumizi chanya na siyo kuiacha ifanye kila kitu,” amesema.
Rugambwa amewataka wasomi wa Afrika kutobweteka kwa kutumia teknolojia za kigeni ambazo siyo salama na maadili, hivyo, waumize vichwa kwa kuzisaidia jamii zao kuja na teknolojia za kwao.
”Teknolojia tunayoitumia ni ya kwetu? kama siyo yetu, tuko salama namna gani, taifa likiwa na teknolojia yake litakuwa limejikomboa. Sisi wasomi kutoka Afrika tuna maoni gani, elimu inatusaidia namna gani kutujenga na kujenga wengine,” amesema Kardinali Rugambwa.
Amewataka wahitimu wa Saut kwenda kuwa mfano bora katika jamii inayowasubiri, wasiridhike bali wapende kujifunza, kuwa wanyenyekevu na kukubali kwamba wao bado ni wajinga kwani elimu haina mwisho.
”Ni matumaini yangu mnakwenda kujenga mstakabali chanya wa taifa na dunia, kujibu changamoto zinazoikabili jamii, msijitenge, mkawe suluhisho la changamoto zilizopo kwa sababu uamuzi wa kanisa kuanzisha vyuo vikuu ilikuwa kusaidia kutoa maarifa kwa watu, kulinda utu wa mtu, na kutengeneza watu ambao watasaidia jamii zao,” amesema Rugambwa.
Naye, Makamu Mkuu wa chuo cha Saut, Padre Profesa Juvenarius AsanteMungu, amesema chuo hicho kinajivunia ubora na uadilifu wa wahitimu wake kwani wamekuwa wakizalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi, maadili, falsafa, na tafakuri tunduizi, ambayo yanawafanya kuwa kituo bora cha kitaaluma.
Amesema katika kuhakikisha chuo hicho kinakuwa na walimu wenye viwango bora kitaifa na kimataifa, mwaka wa masomo 2025/2026 walimu wapya 45 wenye sifa za Shahada ya Udhamiri na Uzamivu wameajiriwa, na walimu 11 wamemaliza masomo yao ngazi hiyo huku wengine wakiendelea na masomo.
”Wahitimu nendeni mkawe mfano bora tunatarajia mtapita njia sahihi ya kusaka maisha, mnapokwenda sokoni nendeni na ujasiri, uvumilivu,mtumie vyema ujuzi mliopata, muwe na uthubutu wa kusimama na kukabili changamoto, mchunge tabia na matendo yenu,” amesema AsanteMungu.
Profesa AsanteMungu amesema katika mwaka wa masomo 2024/2025 baadhi ya wanafunzi wameshindwa kuhitimu masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kukidhi vigezo, matatizo ya kifedha, vifo, na kuchelewa kulipa ada.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema; “Myazingatie yote mliyojifunza hapa, mkawe watoto wema wa kutumainiwa, jamii, familia na nchi yetu inawategemea.”
Mhitimu wa Shahada ya Mawasiliano ya Umma, Beatrice Rabbach amesema licha ya matumizi ya AI kuwa na faidanyingi kwa kuchochea ubunifu, ufanisi na kupunguza muda, ameshauri ni muhimu muongozo ukawekwa vyuoni ili kudhibiti udanganyifu, wizi wa kazi za watu, na matumizi yasiyofaa.
Naye, Shahame Nchimbi, mhitimu wa Shahada ya Sheria, amesema; “Akili Mnemba ni sahihi lakini inategemeana
Wasiiachie akili Mnemba ndo ifanye kazi zote. Akili Mnemba itumike pale inapopswa kwa sababu inatusaidia kwenye kuongeza maarifa.”
