BAADA ya mabosi wa Mbeya City kumkosa kiungo wa Yanga, Farid Mussa dirisha kubwa la usajili lililopita, kwa sasa vigogo hao wamerudi upya kuihitaji saini yake, ikiwa ni harakati za kukisuka kikosi hicho ili kilete ushindani zaidi.
Taarifa kutoka katika timu hiyo zimeiambia Mwanaspoti, Farid ni miongoni mwa wachezaji wanaowindwa na kikosi hicho na tayari kimeanza mazungumzo ya kumpata nyota huyo, ikiwa ni miongoni mwa pendekezo la kocha wa timu hiyo, Mecky Maxime.
“Ni mchezaji tuliyemhitaji tangu dirisha kubwa lililopita ila kuna mambo hayakwenda vizuri na kushindwa kupata saini yake, lengo letu ni kuwapata wachezaji tunaowahitaji mapema ili kuepuka ushindani utakapoanza,” kimesema chanzo hicho.
Mwanaspoti linatambua, Farid mkataba wake unaisha mwakani 2026 na nafasi ya kubakia katika kikosi cha Yanga ni ndogo kutokana na kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara, jambo linaloipa nguvu Mbeya City ya kuanza kuiwinda saini yake.
Farid ni miongoni mwa wachezaji wazawa wenye vipaji vikubwa huku akizichezea timu mbalimbali, zikiwamo za Azam FC, kabla ya kutimkia CD Tenerife B ya Hispania, kisha kurejea nchini na kujiunga rasmi na kikosi hicho cha Yanga Agosti 12, 2020.
Mbeya City inayonolewa na Mecky Maxime aliyechukua mikoba ya Malale Hamsini aliyeipandisha tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, inadaiwa tayari imeinasa saini ya aliyekuwa kiungo wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana.
Maxime aliyewahi kufundisha timu mbalimbali za Kagera Sugar, Dodoma Jiji na Singida Black Stars zamani Ihefu, anahitaji kukisuka upya kikosi hicho dirisha dogo likakalofunguliwa kuanzia Januari Mosi, 2026, ili kuleta ushindani zaidi.