Maximo atoa ya moyoni | Mwanaspoti

ALIYEKUWA Kocha wa KMC, Mbrazil Marcio Maximo amesema hajutii uamuzi uliochukuliwa na uongozi wa timu hiyo wa kusitisha mkataba wake kutokana na mwenendo mbovu wao katika Ligi Kuu Bara msimu huu, huku akibainisha ataendelea kuwapenda na kuwaheshimu.

Kocha huyo aliachana na kikosi hicho Desemba 6, 2025, akiwa amedumu kwa siku 131, tangu alipotambulishwa Julai 28, 2025, baada ya kuiongoza timu hiyo katika mechi tisa za Ligi Kuu, akishinda moja, akitoa sare moja na kuchapwa saba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Maximo amesema licha ya yaliyotokea, lakini kwake ameyapokea kwa mkono mmoja, kwa sababu bado kwa taaluma yake suala la kuondoka sehemu moja kwenda nyingine ni la kawaida, hivyo amechukulia uamuzi huo kiroho safi.

“Ni fahari kwangu kufanya kazi Tanzania kwa sababu ni nchi ninayoipenda, watu wake wanapenda mpira na kiukweli nimeona tangu mara ya kwanza nakuja hapa, Ligi Kuu imepiga hatua, ndiyo maana ni kivutio cha makocha wengi pia,” amesema Maximo.

Aidha, Maximo alisema kwa sasa ni mapema kuzungumzia kama ataamua kupumzika na masuala la ukocha au ataendelea akipata nafasi sehemu nyingine, licha ya baadhi ya klabu mbalimbali za Tanzania na nje ya nchi kuanza mazungumzo naye.

“Nahitaji muda kidogo wa kupumzika kisha baada ya hapo nitafanya uamuzi wa kujua hatima yangu, siwezi kusema sitafanya kazi tena Tanzania au sehemu nyingine, kwa sababu ninachoangalia ni mradi mzuri na mustakabali wangu kijumla,” amesema.

Hii ni mara ya tatu kwa Maximo kuja Tanzania kufundisha soka, baada ya awali kuifundisha Taifa Stars kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, kisha akaifundisha Yanga mwaka 2014, akiwa ni miongoni mwa makocha waliojizoelea umaarufu. Mwaka 2025 akatua KMC.

Maximo alirejea nchini akiwa na kumbukumbu nzuri, kwani ndiye kocha wa kwanza pia kuiongoza timu ya taifa ya Taifa Stars kufuzu Fainali za Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (CHAN), zilizofanyika Ivory Coast mwaka 2009.