Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameonya kuwa upungufu wa maji unaweza kusababisha mgogoro mkubwa kati ya wananchi na Serikali, hali inayoweza kuhatarisha utulivu wa kisiasa na usimamizi wa jiji hilo.
Chalamila ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Desemba 13, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua uzalishaji wa maji katika Mto Ruvu na visima vya kuyahifadhi na kuyasambaza katika eneo la Kimara jijini humo.
“Maji yakikosekana tutazalisha mgogoro mkubwa sana kati ya wananchi na Serikali. Mtu mwenye kiu atawezaje kutii sheria? Kutakuwa na mtikisiko wa kisiasa na jiji halitatawalika,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wajumbe wa bodi za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) na Bodi ya Bonde la Wami–Ruvu kukaa pamoja na kutafuta suluhisho la kudumu la uhaba wa maji unaolikabili jiji hilo.
Katika vyanzo hivyo, Chalamila ameshuhudia jinsi maji yalivyopungua kwa kiwango kikubwa baada ya maeneo unakopita Mto Ruvu kukosa mvua muda mrefu.
Ameonya kuwa iwapo hali itaendelea kwa wiki mbili zaidi bila hatua madhubuti, athari zake zitakuwa kubwa kwa wananchi, viwanda na pato la Taifa.
Chalamila amesema maji yatakayopatikana kutoka Mradi wa Bwawa la Kidunda, ingawa nalo linategemea mvua, yakihifadhiwa na kusimamiwa ipasavyo, yataweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuhudumia wakazi wa Dar es Salaam na kupunguza changamoto ya upungufu wa maji.
Bwawa la Kidunda lililopo mkoani Morogoro, lilianza kujengwa na Serikali mwaka jana na sasa ujenzi wake umefikia asilimia 35, likitarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2026
Mkuu wa mkoa amesema kulingana na maelezo yaliyopewa na wataalamu, Mto Ruvu una tabia ya ukame unaojirudia takribani kila baada ya miaka mitano, hivyo Dawasa kwa kushirikiana na Bodi ya Bonde la Wami–Ruvu, wanapaswa kutafuta suluhisho la kudumu la kukabiliana na hali hiyo.
Ameshauri mipango ya muda mrefu izingatie mabadiliko ya tabianchi na kasi ya ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam, ambalo linakadiriwa kufikia wakazi zaidi ya milioni 10 mwaka 2030.
“Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji saba yanayokua kwa kasi barani Afrika. Ifikapo 2030 litakuwa na zaidi ya watu milioni 10. Ikifika wakati huo, vyanzo vya sasa vya maji vitatosha? Lazima tuangalie mbele,” amesema.
Ameongeza kuwa hata mradi wa Bwawa la Kidunda unategemea mvua ambazo hazitabiriki, hivyo ni muhimu kujiandaa kwa hali ambayo itasaidia ikiwa mvua hazitanyesha labda kwa miaka miwili mfululizo.
Chalamila pia ameunga mkono pendekezo lililotolewa awali na Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkama Bwire, la kutumia maji kutoka Bwawa la Nyerere lililopo Mto Rufiji, akibainisha kuwa mradi huo upo katika hatua za maandalizi ya zabuni.
Vilevile, ameshauri mamlaka za maji kuangalia uwezekano wa kushirikisha sekta binafsi katika hatua za uzalishaji, usafirishaji au usambazaji wa maji, ili kupunguza tatizo linaloongezeka kutokana na ongezeko la idadi ya watu.
Awali, Mkurugenzi wa Bodi ya Bonde la Wami–Ruvu, Elibariki Mmasi amesema hali ya uzalishaji wa maji ni mbaya kutokana na uhaba wa mvua uliodumu kwa miezi saba hadi minane katika maeneo ya Mto Ruvu.
Amesema ili kukabiliana na hali hiyo, bodi imesitisha vibali 250 vya matumizi ya maji kwa shughuli zisizo za majumbani, ili maji machache yaliyosalia yaweze kuwafikia wananchi, japo kwa mgawo.
Vilevile, amesema wanafanya doroa ya mara kwa mara kuhakikisha chanzoi hicho kinalindwa huku wakiandaa maneo mahususi ya wafugaji kunywesha mifugo yao.
