Profesa Mkenda azungumzia kukamatwa mhadhiri UDOM

Moshi. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema taarifa za awali zinaonyesha mhadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) alikamatwa kutokana na matendo aliyofanya nje ya chuo.

Amesema hayo kutokana na taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia jana Desemba 12, 2025 ikieleza mhadhiri wa UDOM amekamatwa chuoni akituhumiwa kwa uchochezi.

Taarifa hiyo iliyosambaa inaonyesha ni barua ya Jumuiya ya Wanataaluma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa) ya Desemba 12, 2025 ikipeleka ujumbe kwa wanachama wake.

Inaelezwa katika barua hiyo kuwa Desemba 9, mmoja wa wafanyakazi alikamatwa, nyumba yake ikafanyiwa upekuzi na akahojiwa kituo cha polisi kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Udomasa, Isaac Mahenge, mfanyakazi huyo ambaye hakutajwa jina alituhumiwa kutoa kauli katika mhadhara wa Desemba 8 (saa 4:30 asubuhi hadi 7:30 mchana) zilizodaiwa kuwachochea wanafunzi kushiriki maandamano ya Desemba 9.

Inadaiwa kauli hizo zilirekodiwa kwa siri na mtoa taarifa aliyekuwapo darasani na kutumwa kwa mamlaka za juu ambazo zilitoa agizo la kukamatwa kwake.

“Tukio hili linaashiria hali mpya ambapo mihadhara inaweza kuwa chini ya ufuatiliaji. Kwa sababu hiyo, tunawahimiza wote kuwa waangalifu mnapokuwa darasani, wakati sisi tukiendelea kuchunguza tukio hili na kubaini hatua zinazofaa kuchukuliwa,” imeeleza barua hiyo ikiwataka kuwa makini.

Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 13, Profesa Mkenda amesema baada ya kuona taarifa hiyo ikizagaa mitandaoni, alifuatilia kwa mamlaka husika kujua ukweli, ambazo zimemweleza zinafuatiliwa.

“Hilo la mhadhiri kwamba amekamatwa kwa sababu ambazo zinatajwa huko ….nimeona kwenye mtandao inazunguka, nimeongea na Waziri wa Mambo ya Ndani, naye amesema analifuatilia japo kwa taarifa ya awali ni kwamba mhadhiri huyo atakuwa amekamatwa kwa sababu ya vitu alivyovifanya nje ya chuo siyo ndani ya chuo,” amesema.

Profesa Mkenda amesema: “Kimsingi, wahadhiri wanapofundisha wana uhuru wa kufundisha lakini kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma zao na siyo kwamba kuna mtu atapeleka polisi akae kwenye chumba aanze kumfuatilia akiwa anafunisha, kama mhadhiri anatoka nje ya mstari wa weledi au maadili ya kazi kuna hatua za kiutawala za kuchukua ndani ya vyuo.”

Amesema kuna mkuu wa idara, makamu wa chuo, wakuu wa vitivo na seneti.

“Hatutarajii kabisa polisi watahusika kwa namna yoyote ile kwenda kusimamia namna ya kufundisha kwenye madarasa yetu, tutakuwa tumeenda mbali sana, hilo halipo,” amesema na kuongeza:

“Wahadhiri tuna wajibu wa kufundisha kwa kuzingatia misingi ya kazi zetu, maadili na weledi. Sitarajii kwamba kutakuwa na usimamizi wa polisi kwenye kusimamia walimu wanapofundisha kwenye vyuo vikuu, endapo mhadhiri atakiuka maadili ya kazi yake, wapo wakuu wa vyuo na taratibu za kiutawala za vyuo zipo.”