CBE kujenga hoteli ya nyota tatu, kampasi Kilimanjaro

Dodoma. Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kinatarajia kutumia jumla ya Sh26.4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hoteli katika eneo la zaidi ya ekari 15 walilopewa, kwa lengo la kuanzisha kampasi ya chuo hicho mkoani Kilimanjaro.

Mbali na kujenga hoteli hiyo inayotarajiwa kuwa ya nyota tatu, chuo kitapata pia majengo ya mabweni, madarasa ya wanafunzi na majengo ya utawala, huku maandalizi ya hatua ya kwanza ya ujenzi tayari yakiwa yameanza.

Kauli hiyo imetolewa leo, Desemba 13, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya CBE, Profesa Zacharia Mganilwa, alipozungumza kwenye mahafali ya 60 ya chuo hicho, ambayo ni ya 42 kwa kampasi ya Dodoma.

Profesa Mganilwa amesema fedha hizo wamezipata kutoka Benki ya Dunia, kwani ilikuwa ni ndoto ya muda mrefu ya chuo kufungua tawi lingine mkoani Kilimanjaro litakalohudumia kanda ya Kaskazini.

Amesema maandalizi yote yamekamilika na tayari Serikali imeshakabidhi ardhi hiyo iliyotolewa na wananchi kwa lengo la kupata tawi la chuo, na wanatarajia hoteli itakayojengwa kuwa sehemu ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wao.

“Tumeaminiwa na kupata fedha hizo, na maandalizi yetu kwa asilimia kubwa tumeyakamilisha, tukiamini tawi la chuo katika kanda ya kaskazini litaanza hivi karibuni. Hii imekuwa hamu yetu ya muda mrefu na sasa ndoto imetimia,” amesema Profesa Mganilwa.

Akizungumza na wahitimu 2,086 waliotunukiwa shahada mbalimbali kuanzia ngazi ya astashahada, stashahada, shahada na shahada ya uzamili, mwenyekiti huyo amewataka kuwa na mawazo zaidi ya moja ili a wazo moja likifeli, lingine lichukue nafasi, badala ya kuangalia wazo moja la kuwa waajiriwa, jambo alilosema haliwezekani kwa wote.

Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga, amesema ndani ya chuo hicho wameanzisha programu kadhaa kulingana na mahitaji ya soko kwa kipindi cha sasa, kwani wanaamini si wahitimu wote watapata ajira, bali wanajenga misingi mizuri ya kujitegemea kwa vijana wao.

Profesa Lwoga amesema chuo hicho kimeshika nafasi ya nane kwa ubora kwa vipindi viwili mfululizo kati ya vyuo 47 nchini, jambo linaloonesha kuwa wako kwenye kiwango kizuri katika utoaji wa elimu kwa Watanzania, ambapo tayari wameanza kutoa elimu masafa kwa ngazi ya shahada ya umahiri.

Akizungumza kwenye mahafali hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, aliyetunuku vyeti kwa wahitimu, amewataka kutumia fursa zinazowazunguka kujitengenezea maisha badala ya kurudi kwa wazazi wao, ambako kutwa nzima wangekuwa wakitazama televisheni.

Senyamule amesisitiza kuwa wahitimu wa vyuo vya Tanzania waache kuwaza ulinganifu wa viwango vya elimu zao na vyuo vya ndani pekee, bali wasome zaidi kwa maarifa, ili wafikirie kushindana na vyuo vya kimataifa, ndipo wapate nafasi za kujua wanahitaji kufanya nini katika maisha ya baadaye.

Chuo cha CBE kilianzishwa Januari 25, 1965 na kuzinduliwa na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, hayati Julius Nyerere, na kwa sasa kina matawi Dodoma, Mwanza na Mbeya, huku kikitarajia kuanzisha tawi jipya mkoani Kilimanjaro.