📍OR-Wizara ya Maendeleo ya Vijana
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka amewaeleza Vijana nia ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuunda Wizara maalum ya vijana ili kukuza ustawi wa kundi hilo.
Waziri Nanauka amesema hayo siku (Disemba,12, 2025) alipokuwa kwenye ziara yake Wilayani Bahi Mkoani Dodoma na kuzungumza na Vijana ambapo amesema kwa sasa asilimia 65 ya watanzania ni vijana chini ya miaka 35 na hivyo kuhitaji kujumuishwa kwenye mipango ya maendeleo.
Aidha, Waziri Nanauka amewataka viongozi wa Halmashauri mbalimbali nchini kuendelea kuwezesha Vijana kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kupitia mapato ya ndani ili vijana waweze kujiajiri na kuajiri vijana wenzao.
Katika hatua nyingine, Waziri Nanauka ametoa kiasi cha Tsh 600,000 kwa ajili ya kuwezesha Wajasiriamali hao kujisajili na kupata vitambulisho vitakavyo wasaidia kutambulika kupitia shughuli wanazofanya ili wavweze kupata mikopo.
Akizungumza awali mjasiriamali wa soko la Bahi Bi Paula Limo ameeleza changamoto wanazokabiliana nazo kama wajasiriamali vijana hususan suala la uwezeshaji mikopo ambapo Waziri Nanauka alishughulikia jambo hilo.
Vile vile, Wajasiriamali hao wa soko la Bahi, wamemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna Serikali anayoongoza imeendelea kushughulikia masuala mbalimbali ya wananchi.