Mbarali. Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya, inatarajia kutumia zaidi ya Sh1 bilioni kwa ajili ya kuboresha maeneo korofi ya miundombinu barabara za pembezoni .
Katika hatua nyingine imeweka mikakati ya kutenga bajeti ya mapato ya ndani kwa mwaka huu wa fedha kwa lengo la kununua mtambo wa kisasa wa kuchonga na kuboresha miundombinu ya barabara.
Hatua hiyo imeelezwa kuhakikisha maeneo muhimu ya sekta ya elimu na kilimo yanafikika ili kuepuka madhara yatokanayo na athari za msimu wa mvua nyingi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbarali, Raymond Mweli amesema leo Jumapili Desemba 14,2025 wakati akizungumza na Mwananchi Digital kuhusiana na miradi mbalimbali wanayo tekeleza kupitia mapato ya ndani.
“Tumejipanga kikamilifu kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati kwa kutumia mapato ya ndani kwenye sekta ya elimu, afya, kilimo, barabara na maji lengo ni kuona tunafikia mipango tuliojiwekea kufikisha huduma kwa wananchi,” amesema.
Mweli amesema kimsingi asilimia 80 ya mapato ya halmashauri inategemea sekta ya kilimo ambapo kwa kipindi cha mwaka 2024/2025, walikusanya Sh10 bilioni na mwaka 2025/2026 malengo ni kukusanya Sh12 bilioni.
“Tumeweka mikakati ya kusaka vyanzo mbalimbali vya mapato ili kufikia kukusanya Sh12 bilioni, lakini kuboresha miundombinu ya kilimo na mazingira wezeshi ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima na ujenzi wa mradi wa skimu 100 za umwagiliaji,” amesema.
Amesema ili kuhakikisha sekta ya kilimo inaboreshwa tayari wamepokea matrekta madogo 76, kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kupitia Wizara ya Kilimo ambayo yataleta tija ya kuongeza uzalishaji.
“Matrekta hayo yatatolewa kwa wakulima wa zao la mpunga, lakini tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa hatua hiyo kubwa kuwekeza nguvu kwenye sekta ya kilimo iliyo na mchango mkubwa kwa pato la Taifa,” amesema.
Mweli amesema zaidi ya migogoro ya ardhi 100 wamepokea ambayo iko katika hatua mbalimbali za utatuzi sambamba na kuanza kurasimisha maeneo na kutoa hati kwa wananchi ili kuondokana na changamoto hiyo.
“Mpaka sasa tayari tumerasimisha maeneo mbalimbali na kutoa hati 14 kwenye taasisi za elimu ili kuepuka changamoto za migogoro ya ardhi inayokwamisha jitihada za Serikali,” amesema.
Mweli ameonya baadhi ya watumishi wa Serikali kutokuwa chanzo cha kuchochea migogoro ya ardhi kwa wananchi wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Mkulima wa zao la mpunga kutoka Kata ya Kapunga, Ester Amos amesema utaratibu wa Serikali kuboresha miundombinu utawasaidia kufikisha zao la mpunga sokoni kwa wakati na kudhibiti walanguzi.
Naye Solomon Oscar, Mkazi wa Madibira wilayani humo, amesema wanaomba mkakati huo wa halmashauri kuboresha miundombinu ufanyike kwa haraka kabla ya mvua za msimu hazijachanganya.
