Moshi. Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka kimepanga kuanzisha programu ya saikolojia katika utalii, itakayolenga kutambua na kuelewa kwa kina malengo, mitazamo na matarajio ya watalii wanaoingia nchini.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha utoaji wa huduma bora pamoja na kuboresha usimamizi endelevu wa sekta ya utalii na uhifadhi wa rasilimali za asili nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Julius Nyahongo, wakati wa mahafali ya 61 ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, yaliyofanyika jana katika viwanja vya chuo hicho, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 649 wamehitimu katika kozi mbalimbali za usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori nchini.
Askari wa Jeshi usu wakiwa kwenye gwaride wakati wa mahafali ya 61 ya chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori. Picha na Janeth Joseph
Profesa Nyahongo amesema kuwa kutokana na mazingira ya kipekee ya utalii yaliyopo nchini, chuo hicho kimejipanga kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kutambua na kuelewa kwa usahihi mitazamo, mahitaji na matarajio ya watalii.
Amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kuboresha utoaji wa huduma katika sekta ya utalii, huku ukiwezesha chuo hicho kuendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya utalii.
“Kwa kuzingatia usalama na amani ya nchi yetu iliyosheheni rasilimali nyingi na za kuvutia, chuo kina mpango wa kuanzisha programu za kuwezesha kuwatambua watalii mbalimbali wanaotembelea nchi yetu kwa ufanisi na kisaikolojia, kwa maana hawa ni sehemu kubwa ya maendeleo ya uchumi wa nchi yetu,” amesema Profesa Nyahongo.
Amesema, “kwa kutambua hili, Chuo kinapanga kuanzisha programu ya saikolojia katika utalii, hii itatuwezesha kuwafahamu wageni wanaofika kwetu, lengo lao, mapenzi yao na mambo mazuri wanayokuja kuona kwetu.”
Pamoja na mambo mengine, amesema chuo hicho kitaendelea kuzalisha wataalamu wa utalii watakaokuwa na uwezo wa kutoa huduma ya dharura kwa watalii wenye changamoto za kiafya wawapo porini au mlimani kabla hawajafikishwa hospitali.
Askari wa Jeshi usu wakiwa kwenye gwaride wakati wa mahafali ya 61 ya chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori. Picha na Janeth Joseph
“Kwa siku za usoni na kutambua kwamba watalii ni binadamu ambao wanaweza kupata changamoto ya kiafya muda wowote, Chuo kina mpango wa kuanzisha programu mpya za uuguzi wa dharura katika utalii na ukarimu, programu ambayo itazalisha wataalamu wa utalii watakaokuwa na uwezo wa kutoa huduma ya dharura kwa watalii wanaopita changamoto wawapo porini au mlimani kabla hawajafikishwa hospitalini,” amesema Profesa Nyahongo.
Aidha, amesema tangu kuanzisha kwa chuo hicho mwaka 1963, kimefanikiwa kuzalisha wataalamu zaidi ya 12,000 katika nyanja za uhifadhi wa wanyamapori na utalii kutoka katika nchi 28 za bara la Afrika na 26 nje ya bara la Afrika.
Akizungumza katika mahafali hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande, amesema Serikali kupitia programu maalumu imepanga kusomesha bure vijana 100 waongoza watalii ili kuwapa ujuzi na taaluma inayowawezesha kutoa huduma bora kwa watalii, na hivyo kuvutia watalii zaidi kuitembelea nchi.
Aidha, amewataka wahitimu hao kwenda kulitumikia Taifa kwa kufanya kazi zao kwa uadilifu, uzalendo na kwa unyenyekevu wa hali ya juu na kuepuka tamaa.
