Songea. Aliyekuwa Mbunge wa Peramiho (CCM), marehemu Jenista Mhagama, ametajwa kuwa zawadi ya Mungu kwa watu, hususan maskini, wasiojiweza na watu wenye ulemavu, kutokana na maisha yake ya kujitoa kwao bila kuchoka.
Hayo yamesemwa leo, Jumapili, Desemba 14, 2025, kqtikq mahubiri yaliyotolewa na Padri Josephat Ngonyani wa Kanisa Katoliki Litapwasi, wakati wa ibada takatifu ya kumuombea marehemu.
Amesema Jenista aliishi maisha ya imani, unyenyekevu na upendo kwa watu, akimtumikia Mungu kwa vitendo.
Padri Ngonyani amesema marehemu aliwapenda watu na kanisa, akisisitiza alikuwa mtu wa sala, sadaka na kujitoa, huku akiwahimiza waombolezaji kutoogopa kifo bali kujikabidhi kwa Mungu na kuiga mfano wa maisha ya marehemu.
“Jenista alituonya tusiogope kifo, bali tumtumainie Mungu. Alimwona Mungu katika watu aliowatumikia,” amesema Padri Ngonyani.
Ameongeza enzi za uhai wake, Jenista aliposhika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo Waziri wa Afya, aliwasaidia wagonjwa wengi kwa kuhakikisha wanapata matibabu, hata wale wasiokuwa na uwezo wa kifedha.
Padri Ngonyani amesema marehemu alikuwa mtoaji mkubwa wa sadaka na michango ya kanisa, akitaja mchango wa Sh10 milioni alioutoa kufanikisha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 125 ya Kanisa, akisema hakuwa nyuma katika kazi za Mungu.
Katika mahubiri yake, amewahimiza waumini kuvumilia changamoto za maisha na kutokata tamaa hata wanapokutana na maanguko au kukataliwa.
“Jenista alitufundisha unyenyekevu kwa wakubwa na wadogo, kuthamini watu na kuwaombea. Leo amelala, lakini ujumbe wake ungelikuwa mmoja—tupendane,” amesema.
Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, amesema Jenista Mhagama alizaliwa Juni 23, 1967, katika Kijiji cha Parangu, Peramiho, mkoani Ruvuma.
Alipata elimu ya msingi Parangu na kuendelea na elimu ya sekondari kuanzia mwaka 1982 hadi 1985, kabla ya kujiunga na Chuo cha Ualimu Korogwe, ambako alihitimu masomo ya ualimu.
Mwaka 1999, alipata Shahada ya Kwanza ya Uongozi na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge, na hadi anafariki dunia alikuwa akiendelea na masomo ya Shahada ya Uzamili (Masters) kwa njia ya masafa nchini Uingereza.
Kwa upande wa ajira, Jenista alianza kazi mwaka 1990 hadi 1997 akiwa mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Songea. Kisha aliingia kwenye siasa, akichaguliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kuanzia 2000–2005, na baadaye Mbunge wa Peramiho kuanzia 2005 hadi 2025.
Aidha, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwemo Naibu Waziri wa Elimu (2014–2015) na baadaye Waziri wa Afya (2024–2025).
Watoto wa aliyekuwa Waziri wa Afya Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Peramiho . Jenista Mhagama wakiwa kwenye Misa ya kumuombea Mama yao iliyofanyika kwenye kanisa katoliki Matogoro Manispaa ya songea . Picha na Joyce Joliga
Jenista Mhagama alifariki dunia Desemba 11, 2025, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu maradhi ya moyo, baada ya kuugua ghafla.
Mwili wake unatarajiwa kusafirishwa leo kutoka nyumbani kwake Makambi, Manispaa ya Songea, kwenda Kijiji cha Parangu, Peramiho, ambako waombolezaji na wananchi wa jimbo lake watapata fursa ya kumuaga kesho Jumatatu.
Baadaye Jumanne ya Desemba 16, 2025, mwili wake utasafirishwa kwenda Kijiji cha Ruanda, nyumbani kwa marehemu mumewe, kwa ajili ya mazishi siku hiyohiyo.
