Hatma ya kiungo Mnigeria ipo kwa Maxime

UONGOZI wa Mbeya City huenda ukaachana na mpango wa kumtema kiungo Mnigeria, Paschal Onyedika Okoli katika dirisha dogo la Januari mwakani, baada ya awali nyota huyo kudaiwa hana furaha kutokana na kutocheza kikosi cha kwanza mara kwa mara.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo umeliambia Mwanaspoti, kiungo huyo aliyebakisha miezi sita katika mkataba wake, kwa sasa ataendelea kusalia, wakiendelea kuangalia na kupitia pia ripoti ya benchi la ufundi chini ya kocha Mecky Maxime.

“Baada ya kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi, kwa sasa hatuangalii ripoti iliyopita kwa sababu tuna kocha mpya anayehitaji kuangalia kila mchezaji, lengo letu kubwa ni kuboresha na sio kuvuruga kikosi,” alisema kiongozi huyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota, alisema mchezaji huyo ataendelea kusalia ndani ya kikosi hicho, kwani hadi sasa uongozi wa timu hiyo unaridhishwa na kiwango anachoendelea kukionyesha.

“Suala la kuachana naye hilo halipo kwa sasa kwa sababu bado ni mchezaji mzuri tunayeamini anaweza kutusaidia mbele, tuna benchi jipya la ufundi linalohitaji kumuona kila mmoja wao, hivyo, sio rahisi kama inavyosemwa,” alisema Gwamaka.

Nyota huyo aliyezaliwa Oktoba 17, 1997 amejiunga na kikosi hicho msimu huu baada ya kuachana na Klabu ya NK Celik Zenica ya Bosnia and Herzegovina, akiwahi kuichezea pia Bursaspor ya Uturuki, kuanzia ngazi ya timu za vijana hadi ya wakubwa.

Mbeya City inayonolewa na Mecky Maxime aliyechukua mikoba ya Malale Hamsini aliyeipandisha tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka kwa msimu wa 2022-23, inadaiwa tayari imeinasa saini ya aliyekuwa kiungo wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana.