BEKI kisiki wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania, Noela Luhala amevunja mkataba na klabu ya 1207 Antalya Spor ya Uturuki kwa makubaliano ya pande mbili na kwa sasa anajiandaa kutimkia Lithuania katika dirisha lijalo la usajili wa majira ya baridi.
Noela ambaye alitua Uturuki Septemba mwaka huu, amefikia makubaliano ya kuvunja mkataba na Antalya baada ya kupata ofa nono kutoka kwa MFA Zalgiris ya Lithuania.
Akiwa na Antalya tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi nane za Ligi Kuu Uturuki na anaiacha timu hiyo ikiwa katika nafasi ya 13 katika msimamo unaohusisha klabu 16.
Noela alianza maisha yake ya soka la kulipwa Israel msimu uliopita ambapo alisajiliwa na Asa Tel Aviv kwa mkataba wa mwaka mmoja na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu.
Baada ya kumaliza mkataba wake na vigogo hao wa Israel aliamua kwenda kutafuta changamoto mpya Uturuki ambako amedumu kwa miezi minne kabla ya kuvunja mkataba siku chache zilizopita baada ya Zalgiris kupiga hodi.
Zalgiris ni kati ya timu tishio huko Lithuania kwani msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya FC Gintra iliyobeba ubingwa kwa tofauti ya pointi 11.
Staa huyu wa Twiga aliyekuwa nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania cha umri chini ya miaka 17, kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyikia India, anaingia katika rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza soka la kulipwa Lithuania akiungana na baadhi ya mastaa wengine wa Afrika ambao wamewahi kupita katika ligi hiyo hapo awali na kwenda kufanya makubwa baadae kama Jermaine Seoposenwe ambaye kwa sasa anaitumikia Monterrey inayoshiriki Ligi Kuu Mexico.
