Bibi kizimbani, akidaiwa kusafirisha bangi

Dar es Salaam. Mkazi wa Mbezi Msigani, Salma Said (60), maarufu Nangwe amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka la kusafirisha gramu tatu za dawa za kulevya aina ya bangi.

Mshtakiwa amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu Desemba 15, 2025 na kusomewa kesi ya jinai na wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling’i.

Mbiling’i amedai mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga kuwa mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja na kisha kumsomea shtaka hilo.

Wakili Mbiling’i amedai Juni 28,2025, eneo la Mbezi Msigani, wilaya ya  Ubungo, mshtakiwa alikutwa alisafirisha gramu 3.8 za dawa za kulevya aina ya bangi, kinyume cha sheria.

Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo alikana kuhusika na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi umekamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea hoja za awali (PH).

Upande wa Jamhuri umedai kiasi cha dawa alizoshtakiwa nacho kina dhamana na waliomba mahakama itoe masharti yatakayomfanya mshtakiwa ahudhurie mahakamani hapo kila kesi yake itakapotajwa.

Hakimu Mwankuga alikubaliana na upande wa mashtaka na kutoa masharti matatu ya dhamana dhidi ya Salma ambayo ni mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye kitambulisho cha Taifa( Nida).

Pia wanatakiwa wawe na barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa wanapoishi au barua ya mwajiri kama ni mfanyakazi.

Hakimu Mwankuga pia aliwataka wadhamini hao kusaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja na kuhakikisha mshtakiwa anahudhuria kesi mahakamani hapo bila kukosa.

Mshtakiwa amefanikiwa kutimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana, ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 15, 2026.