Bukoba. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi ametoa wito kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuhakikisha Kampasi mpya ya Mkoa wa Kagera inakuwa kitovu cha uvumbuzi na ubunifu ili kuwawezesha vijana kutumia fursa za soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumatatu, Desemba 15, 2025 alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kampasi ya UDSM, Mkoa wa Kagera, inayojengwa katika Kijiji cha Itawa wilayani Bukoba.
Ujenzi huo wenye thamani ya Sh14 bilioni, unakifanya kuwa chuo kikuu cha kwanza cha umma kujengwa katika mkoa huo ambao unasifika kwa kutoa wasomi wengi nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi akisikiliza maelezo kutoka kwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Bernadeta Killian kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mkoa wa Kagera, wakati wa uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo hicho leo Desemba 15, 2025 katika Kijiji cha Itawa mkoani Kagera.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla hiyo, Dk Nchimbi amesema mradi huo hauhusu tu miundombinu, bali ni maandalizi ya nguvu kazi ya baadaye ya Tanzania.
Amesema, chuo hicho kihakikishe mitalaa itakayotumika katika kampasi hiyo inalenga moja kwa moja katika kuleta maendeleo ya jamii kwa kutoa zaidi elimu-ujuzi, yaani mafunzo ya amali, kwa kuwa Mkoa wa Kagera na kanda yote ya ziwa ina fursa nyingi za kiuchumi.
“Elimu, hasa elimu ya juu, ina mchango mkubwa sana katika kuzalisha rasilimali watu ya Taifa,” amesema Dk Nchimbi.
“Uwekezaji huu unalenga kuhakikisha vijana wetu wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya uchumi na maendeleo ya taifa.”
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi akiwa pamoja na viongozi mbalimbali, akiweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mkoa wa Kagera, leo Desemba 15, 2025.
Makamu wa Rais amesema, kwa kuwa Mkoa wa Kagera unapakana na nchi jirani kadhaa, uwepo wa kampasi hiyo utatoa fursa na kuvutia vijana katika nchi hizo kuja kujipatia maarifa muhimu.
Amesisitiza kampasi hiyo iwe ni mahali pa kukuza mtangamano wa Afrika Mashariki na kuendeleza umajumui wa Afrika ambao umekuwa msukumo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Vilevile, amesema ni tumaini kupitia kampasi hiyo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitatoa mchango mkubwa katika kuendeleza maarifa katika ujasiriamali, kukuza ujuzi wa masoko, kuchochea biashara za mpakani na kujenga uwezo wa vijana kuhimili ushindani katika soko la kikanda na kimataifa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi akisalimiana na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye ni Rais Mstaafu wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete wakati alipowasili katika Kijiji cha Itawa mkoani Kagera, katika uwekaji wa Jiwe la Msingi la ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mkoa wa Kagera leo Desemba 15, 2025.
Chuo hicho kinajengwa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kutekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mradi huo umebuniwa kuboresha vyuo vikuu, kupanua fursa za elimu na kuoanisha ufundishaji pamoja na tafiti na mahitaji ya soko la ajira.
Ujenzi utajumuisha kumbi za mihadhara, madarasa, maabara za kompyuta, ofisi za wafanyakazi, mabweni ya wanafunzi na miundombinu ya huduma nyingine.
Kinatarajiwa kupokea wanafunzi 660 katika awamu ya kwanza, kikianza na programu za biashara na Tehama, huku mipango ikiwa ni kuongeza idadi ya wanafunzi hadi 1,200 ndani ya miaka mitatu.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema utambulisho wa mkoa huo umefungamana kwa karibu na elimu.
“Utambulisho wa wazee wa mkoa huu unaonekana katika viwango vya elimu walivyofikia,” amesema Kikwete. “Karibu kila kijiji utamkuta profesa, na kama si profesa basi mtu mwenye shahada ya uzamivu (PhD).”
Amesema kukosekana kwa kampasi ya chuo kikuu cha umma kwa muda mrefu kulikuwa kunapingana na urithi huo wa kielimu.
“Kwa kutambua hitaji kubwa la chuo kikuu, Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza kuleta kampasi ya UDSM hapa,” amesema. “Jukumu lenu sasa ni kuhakikisha wanafunzi wanakuja na kutenga ardhi zaidi kwa ajili ya upanuzi wa baadaye.”
Kikwete pia amesisitiza UDSM ina wajibu wa kulinda viwango vya kitaaluma kadri inavyoendelea kupanuka.
“Tumejizatiti kutoa elimu ya juu yenye ubora wa kimataifa,” amesema. “Hatutaki wahitimu ambao wanapokwenda nje ya nchi wanaonekana kama wana shahada zinazolingana na stashahada. Lazima elimu yetu iendane na mahitaji ya dunia ya sasa.”
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema chuo cha Kagera kinaakisi mabadiliko ya sera yaliyoelekezwa na Rais Samia ili kukomesha tofauti za kikanda katika upatikanaji wa elimu ya chuo kikuu.
“Mradi ulipoanza, lengo lilikuwa kuboresha zaidi kampasi na vituo vilivyokuwapo,” amesema Profesa Mkenda. “Lakini Rais alielekeza kuwa vyuo vikuu visambazwe hadi maeneo ambayo hayakuwa yamefikiwa.”
“Kila mkoa ulikuwa na matawi ya Chuo Kikuu Huria, lakini haukuwa na vyuo vikuu vya umma. Rais alielekeza vyuo vikuu visambazwe katika kanda zote za nchi.”
Mchambuzi wa masuala ya elimu na mwalimu mstaafu, James Rutashobya, amesema ujio wa UDSM unaweza kusaidia kupunguza uhamaji wa wanafunzi na rasilimali kwenda mikoa mingine.
“Kwa miaka mingi, wanafunzi wetu bora walilazimika kuondoka Kagera kwenda kusoma elimu ya juu. Kampasi hii inabadilisha hali hiyo na kuleta fursa mpya kwa familia na wafanyabiashara,” amesema.
