KLABU ya KVZ inayoshiriki Ligi Kuu Soka Zanzibar, imemtambulisha Malale Hamsini kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, huku ikielezwa anakwenda kuongeza nguvu kwa kushirikiana na Ali Khalid Omar.
Katika taarifa yao, KVZ imesema: “Karibu nyumbani kwa mabingwa kocha Malale Hamsini.”
Malale ametua KVZ baada ya Novemba 30, 2025 kusitishiwa mkataba kwa makubaliano ya pande mbili na Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, kufuatia mwenendo mbovu wa timu hiyo katika kusaka matokeo mazuri.
Ndani ya KVZ, Malale ana kibarua kikubwa cha kufanya timu hiyo ibebe ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar kwani tangu kuanzishwa kwa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) haijawahi kuchukua, huku msimu uliopita 2024-2025 ikimaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi 62 sawa na Mlandege iliyochukua ubingwa kwa tofauti ya mabao.
Hivi sasa Malale ana kazi ya ziada kuirudisha KVZ kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kufuatia kushushwa na Zimamoto hadi nafasi ya tatu baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Mao, Mjini Unguja, Desemba 13, 2025.
Leo Desemba 16, 2025 saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa Mao A, KVZ yenye pointi 23 ikishika nafasi ya tatu, itashuka dimbani kucheza dhidi ya Mlandege iliyopo nafasi ya nane na pointi 18, zote zikicheza mechi 12.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana msimu wa 2024-2025, KVZ iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mlandege, mechi iliyochezwa siku mbili kufuatia mvua kubwa iliyonyesha na kufanya uwanja wa Mao kujaa maji. Kipindi cha kwanza kilichezwa jioni na dakika 45 za kipindi cha pili kumaliziwa saa nne asubuhi siku iliyofuata.
