WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa viwanja vya michezo unaoendelea katika Mkoa wa Kusini Pemba.
Waziri Pembe amesema hayo leo Desemba 16, 2025 katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa viwanja vya michezo katika Wilaya za Unguja na Pemba.
“Miradi inaendelea vizuri na changamoto zinazojitokeza haziwezi kuepukika ikiwemo mvua, lakini tumekaa pamoja na wadau na kuzitafutia ufumbuzi,” amesema Pembe.
Aidha, amesema Serikali imefanya maboresho makubwa katika miundombinu ya michezo na kusisitiza kuwa ujenzi huo unapaswa kuendana na kasi ya Serikali.
Vilevile, ameshukuru washauri elekezi pamoja na makandarasi kwa juhudi zao na kuwataka kuongeza kasi ya ujenzi ili kukabidhi viwanja kwa wakati waliokubaliana.
Kwa upande wake, Meneja wa Uwanja wa Gombani, Nassir Salim Ali, amesema ujenzi wa uwanja huo umewezesha zaidi ya vijana 500 kupata ajira.
Naye Sheha wa Shehia ya Kichungwani, Yussuf Saleh Salim, ameomba Serikali kujenga uzio wa Kiwanja cha Tenisi ili kukilinda dhidi ya uharibifu.
“Kiwanja cha Tenisi ni roho ya Mji wa Chake Chake, kwani vijana wengi kutoka maeneo mbalimbali huja kushiriki michezo tofauti na kimeibua vipaji vingi vya michezo,” ameeleza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Skuli ya Msingi Ukutini, Idrisa Khamis Vuai, ameishukuru Serikali kwa juhudi zake za kujenga viwanja vya michezo, akisema vitasaidia watoto na vijana kugundua na kukuza vipaji vyao.
