Tumaini elimu ya ufundi stadi kuunganishwa na miradi ya kimkakati

Dar es Salaam. Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan akieleza mpango wa Serikali kuongeza programu maalumu za mafunzo ya ufundi stadi kupitia vyuo vya ufundi na kuziunganisha moja kwa moja na miradi mikakati ya taifa, imeibua mjadala mpana miongoni mwa wadau wa elimu, wataalamu wa masoko ya ajira, na vijana wenyewe.

Kauli hiyo aliyoitoa katika hotuba yake ya kufungua Bunge la 13 imeonekana kama hatua ya kimkakati ya kujenga rasilimali watu imara, huku ikipokelewa na wengi kama kigezo muhimu cha kuligeuza Taifa kuwa kitovu cha utaalamu wa kisasa Afrika Mashariki.

Katika mpango huo, vyuo vya ufundi stadi vitaanza kutoa mafunzo yanayolenga moja kwa moja sekta za reli ya kisasa (SGR), ujenzi na uendeshaji wa bandari, uchumi wa buluu, pamoja na maeneo yanayochipukia ya madini na gesi.

Uamuzi huu unatajwa na wadau kama mwanzo wa mapinduzi katika mfumo wa utoaji elimu ya ufundi nchini, wakieleza kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kutengeneza nguvu kazi inayoendana na uhalisia wa miradi ya kimaendeleo.

Kwa muda mrefu, changamoto kubwa katika soko la ajira nchini imekuwa pengo kati ya kinachofundishwa shuleni na ujuzi unaohitajika katika ajira halisi.

Wataalamu wanasema vijana wengi wamekuwa wahitimu bila uwezo wa vitendo, hali iliyosababisha kampuni nyingi ikiwamo zinazotekeleza miradi mikubwa kuajiri wataalamu kutoka nje.

Kwa mujibu wa Anna Mshana, mtaalamu wa elimu ya ufundi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema katika mazingira ambayo dunia inaingia kwenye uchumi unaotegemea ujuzi wa vitendo, hatua ya kuunganisha mafunzo ya ufundi stadi na miradi mikakati ni hatua ya kimkakati, ya kisasa, na yenye tija ya muda mrefu.

Anasema hatua hiyo itapandisha hadhi ya mafunzo ya ufundi stadi kutoka ngazi ya chini hadi kuwa injini ya maendeleo ya kiuchumi.

“Miradi kama SGR, uchumi wa bahari na sekta ya gesi inahitaji wataalamu waliobobea. Endapo vyuo vya ufundi vitafunguliwa na kuunda mitalaa maalumu kwa ajili ya miradi hiyo. Tanzania inaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa utegemezi wa wataalamu wa nje,”anasema Anna.

Mtaalamu wa elimu ya ufundi kutoka katika mojawapo ya vyuo vya ufundi jijini Dar es Salaam, Tumaini Mhando anasema mpango huu ndio hatua iliyokuwa inahitajika kwa muda mrefu ili kuvunja ukuta kati ya mitalaa ya ufundi na mahitaji ya sekta ya viwanda.

Kwa miaka mingi tumezalisha wanafunzi wa nadharia zaidi kuliko vitendo. Kuunganisha vyuo vya ufundi na miradi mikubwa kutabadilisha kabisa mfumo wa uzalishaji nguvu kazi. Vijana watakuwa sehemu ya miradi mikakati kabla hata hawajahitimu,”anasema.

Anapendekeza pia Serikali kuweka utaratibu wa ulazima wa mafunzo katika maeneo ya kazi kwa wanafunzi wa ufundi ili kuwapima katika mazingira halisi ya kazi.

Mbali na hilo uamuzi huo umetajwa kuwa hatua madhubuti katika kukabiliana na changamoto ya ajira  kwa vitendo.

Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali za ajira, asilimia kubwa ya vijana wanaohitimu vyuo vya kati na vya juu hukaa kwa  miaka kadhaa bila kupata ajira.

 Hii imekuwa chanzo cha kukatisha tamaa na mara nyingi imechangia vuguvugu la vijana kujitumbukiza katika shughuli zisizo rasmi au za uwezekano mdogo wa kipato endelevu.

Lakini vijana wengi wameonekana kupokea kwa matumaini uamuzi wa Serikali kuhamishia mafunzo katika mazingira halisi ya kazi.

Grace Kimaro, mhitimu wa ngazi ya cheti kutoka VETA anasema hatimaye vijana wanaweza kuamini kuwa wanachojifunza kina dhamana ya ajira tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wao wanabahatisha.

“Tulikuwa tunasoma nadharia nyingi sana, lakini ukifika kwenye kampuni unakutana na mitambo ya aina tofauti kabisa. Ukifanya mafunzo ya vitendo kwenye mradi halisi, unakuwa tayari una uwezo mkubwa kuliko anayejifunza bila kuona uhalisia,” anasema.

Vijana wengi waliomaliza vyuo vya ufundi wameonyesha matumaini makubwa, wakisema hatua hiyo ni uthibitisho kuwa Serikali imeanza kusikiliza sauti yao.

Daniel Mollel, kijana kutoka Kigoma aliyesoma ufundi bomba, anasema mara nyingi alikataliwa kwenye kazi kwa sababu hakuwa na uzoefu wa kufanya kazi kwenye mitambo mikubwa.

“Waajiri wanataka mtu aliyeshawahi kushika mashine halisi. Sisi tuliotoka vyuoni tulijifunza kwa nadharia nyingi na maabara chache. Kama programu zitatuunganisha na mradi kama ule wa bomba la mafuta, basi tutakuwa tumefunguliwa mlango ambao tulikuwa tunausukuma bila mafanikio,” anaeleza.

Kwa upande mwingine, Scolastica Mwakyusa, mwanafunzi wa mwaka wa pili chuo cha VETA Mbeya, anasema hatua hiyo inaweza kuongeza hamasa kwa wasichana wengi kuingia kwenye fani za ufundi.

“Wanawake tumezoea kusikia sekta hizo ni za wanaume. Lakini ukituonyesha kampuni kubwa zinazotuhitaji, hata sisi tunaweza kuingia na kufanya vizuri. Serikali ikituweka kwenye miradi mikubwa tutashindwa nini?” anahoji.

Kwa miaka mingi, elimu ya ufundi imeonekana na baadhi ya wazazi na wanafunzi kama fursa ya ‘waliokosa’ nafasi vyuo vikuu. Lakini mwelekeo huu mpya umeanza kuondoa dhana hiyo polepole.

Kwa mujibu wa mhandisi George Mollel, anayefundisha kozi za umeme viwandani Dar es Salaam, kuhusishwa kwa vyuo vya ufundi na miradi ya kimkakati kutabadili mtazamo wa jamii.

Kama taifa linawekeza katika kutoa wataalamu wa reli, bandari, bahari, gesi na madini kupitia ufundi stadi, jamii italazimika kukubali kuwa elimu hii si ya daraja la pili. Kote duniani, taifa lenye mafundi bora ndilo linalosonga mbele,” anasema.

Licha ya kupongeza wadau wa elimu wanasema mpango huo wa kuunganisha mafunzo ya ufundi stadi na miradi mikubwa ya kimkakati yatategemea mambo muhimu ambayo yana hitaji umakini wa karibu.

Wanasema bila kuyashughulikia ipasavyo mambo hayo mpango huo unaweza kukwama au kutoa matokeo yasiyolingana na matarajio ya Taifa.

Miongoni mwa mapendekezo yao ni uongezaji wa  vifaa vya kisasa kwenye vyuo hivyo, ili kuhakikisha teknolojia inayofundishwa inaendana na mahitaji ya sasa ya viwanda na miundombinu.

Asha Lulambo ambaye ni mwalimu wa ufundi anasema ili kupata matokeo chanya kwenye mpango huo, Serikali haina budi kufanya uwekezaji mkubwa kwenye vifaa vya ufundi ili wanafunzi wajifunze kwa ubora ule unaohitajika kwenye miradi.

Anasema bila uwekezaji huu, mafunzo yatabaki kwenye nadharia, na pengo kati ya mitalaa na uhalisia wa kazi litaendelea kuwa kubwa.

“Mitalaa inaweza kurekebishwa, lakini kama vifaa vya kisasa havipo, bado tutakuwa tunazalisha vijana walio na ufa wa uwezo. Miradi mikakati inahitaji mitambo ya kisasa, na vyuo navyo vinapaswa kuwa na mitambo hiyo

“Hatuwezi kumtengeneza fundi wa reli ya kisasa kwa kutumia vifaa vya miaka ya 1980. Hatuhitaji ahadi tu, tunahitaji uwekezaji mkubwa katika maabara, mitambo, warsha na vifaa vya kisasa vinavyolingana na mazingira ya kazi halisi.”anabainisha.

Eneo lingine ambalo limetakiwa kupewa kipaumbe ili kufanikisha mpango huo ni ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na kampuni zinazotekeleza miradi mikubwa ili vijana kuwa na wigo mpana wa kupata mafunzo kwa vitendo.

Pascal Mikwabe ambaye kitaaluma ni ofisa rasilimali watu anasema mafunzo ya vitendo hayawezi kufanikiwa bila kampuni kuruhusu wanafunzi kuingia kwenye maeneo ya kazi, kushika mitambo na kujifunza kwa wataalamu waliopo.

“Kampuni zinapaswa kufanya kazi pamoja na vyuo kutengeneza mitalaa, kupanga ratiba za mafunzo, kutoa wakufunzi wa muda, na kusaidia vifaa vinavyolingana na teknolojia tunayotumia.”anasema Mikwabe.

Motisha kwa wakufunzi na wataalamu wa mafunzo ya ufundi nayo inatajwa kama kitu muhimu kinachoweza kuongeza chachu kwenye mpango huo wa kuunganisha mafunzo ya ufundi stadi na miradi ya kimkakati.

Wadau pia wanasema hakuna mageuzi yatakayofanikiwa bila kuwekeza kwa wakufunzi wenyewe huku vyuo vingi vinakabiliwa na upungufu wa wakufunzi wenye utaalamu wa kisasa, huku wengine wakifanya kazi katika mazingira magumu bila motisha ya kutosha.

“Kama mwalimu wa ufundi hana mafunzo endelevu, hana semina za kuboresha uwezo, hana vifaa vya kufanya utafiti au majaribio, basi hatoweza kumfundisha kijana stadi za kisasa.

“Mwelekeo huu kama utawekewa bajeti, ufuatiliaji na dhamira ya dhati ya usimamizi, unaweza kuwa balozi wa Tanzania mpya yenye vijana wanaojitegemea, wanaojiajiri na wanaoweza kushindana katika soko la ajira duniani.”anasema mwalimu wa chuo cha ufundi ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.