Arusha. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta ya bandari nchini yametokana na uwekezaji wa kimkakati uliofanywa na Serikali.
Alisema ufanisi wa uhudumiaji wa shehena mbalimbali katika bandari zinazosimamiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) umeendelea kuongezeka, huku Bandari ya Dar es Salaam ikionesha mafanikio makubwa zaidi.
“Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, bandari hiyo imefanikiwa kuongeza kiwango cha shehena kinachohudumiwa kwa zaidi ya asilimia 36 kwa mwaka, kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwa bandari hiyo.
“Ongezeko hilo limechangiwa na maboresho ya miundombinu, matumizi ya vifaa na teknolojia za kisasa pamoja na kuimarishwa kwa mifumo ya uendeshaji, hatua ambazo zimeongeza ufanisi wa utoaji huduma na kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango muhimu la biashara kwa nchi jirani na ukanda mzima,” alisema.
Kihenzile alisema hayo jana jioni wakati akifungua mkutano wa 18 wa tathmini ya utendaji wa sekta ya uchukuzi uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Alisema uwekezaji huo umeleta mageuzi makubwa katika uendeshaji wa bandari na kuongeza ufanisi wa huduma kwa watumiaji wa bandari ndani na nje ya nchi.
Kihenzile alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, zaidi ya tani milioni 34 za shehena zinahudumiwa kupitia bandari zote za mwambao wa Bahari ya Hindi pamoja na bandari za Maziwa Makuu.
Alisema kiwango hicho kinaonesha ongezeko kubwa la uwezo wa bandari nchini katika kupokea na kuhudumia mizigo kwa ufanisi.
Kihenzile ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya bandari, matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na maboresho ya mifumo ya uendeshaji.
“Hatua hizo zimepunguza muda wa kuhudumia meli na mizigo, kuongeza ushindani wa bandari za Tanzania na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi wa taifa,” alisema.
Amefafanua kuwa Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya upanuzi na uboreshaji wa bandari ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, pamoja na maboresho ya bandari za maziwa.
Alisema matumizi ya vifaa vya kisasa na mifumo ya Tehama yamepunguza muda wa kuhudumia meli na kuongeza ushindani wa bandari za Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, alisema kasi ya ukuaji wa bandari nchini si ya kawaida, akieleza kuwa kwa sasa bandari zimekuwa zikiongezeka kwa kiwango cha takribani asilimia 36 kwa mwaka.
Profesa Kahyarara ameongeza kuwa ushindani katika sekta ya bandari ni jambo muhimu kwa maendeleo, kwani huchochea taasisi na wadau kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, kuboresha huduma na kuwekeza zaidi katika miundombinu na teknolojia.
Amesema kupitia ushindani huo, bandari za Tanzania zimeendelea kujiimarisha na kuwa na uwezo wa kushindana na bandari nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.