Mashabiki Simba, Yanga kuonyeshana umwamba

Mashabiki wa Simba na Yanga watacheza mechi ya kirafiki, Jumapili, Desemba 21, 2025 kwa lengo la kuhamasisha upendo na umoja baina yao.

Mechi hiyo itachezwa katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni na hakutakuwa na kiingilio kwa mashabiki.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amewaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi katika mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

“Mchezo huu unabeba hadhi ya taasisi husika. Jambo hili lina baraka za mamlaka zote kwa maana ya serikali, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini na klabu hizi mbili za Simba na Yanga. Tunaiita mechi ya kiushindani kwa sababu lazima timu moja ifungwe na mshindi apate zawadi.

“Kuanzia hivi sasa, timu zote mbili zitaingia kambini kujiandaa na mchezo huo na kila upande unapaswa kuitazama mechi hii kama nyingine muhimu katika maisha yao,” amesema Ahmed Ally.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe amesema kuwa mechi hiyo ina maana kubwa kwa taswira ya soka Tanzania. 

Maono ambayo tuko nayo, hili jambo liwe la kudumu. Tunatamani liwe na kila mwaka. Tuwe na tamasha ambalo linatukutanisha mashabiki wa klabu hizi kubwa na klabu mbalimbali Tanzania.Dhumuni kubwa ya jambo hili ni kuwaonyesha watu wote wenye mashaka kwamba Simba na Yanga wameshavuka kwenye utani wao, kwamba jambo hilo sio kweli.

“Sisi ni ndugu, tunakaa na kutembea pamoja. Jambo hili linatuhusu wote ambao tunapenda mpira. Kwenda kuipanda mbegu hii ya utani wa jadi, tarehe 21 mwaka huu. Tunawaomba mashabiki wa mpira kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa KMC kusapoti jambo hili.

“Tuko kizazi hiki, kuna kizazi kingine ambacho kitakuja baada ya hiki, kinatakiwa kione sura ya utani wa jadi wa timu hizi,” amesema Kamwe.