Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji ameteua mwenyekiti na wajumbe wa Bodi ya ushauri ya Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 5(4) cha Sheria ya Wakala wa Serikali, Sura ya 245.
Taarifa ya uteuzi huo, imetolewa leo Jumanne, Desemba 16, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi.
Imeeleza uteuzi huo unalenga kuimarisha uongozi na usimamizi wa kitaaluma wa chuo hicho, sambamba na juhudi za Serikali za kuongeza ubora wa mafunzo katika sekta ya utalii inayokua kwa kasi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk Kijaji amemteua Dk Sharifa Salim kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya NCT.
Wajumbe wengine walioteuliwa ni Enock Wagala, Dk Ladislaus Batinoluho, Plasdius Mbossa na Zainabu Ansell. Aidha, Dk Florian Mtei ameteuliwa kuwa Katibu wa Bodi hiyo.
Taarifa hiyo, imeeleza bodi hiyo ina jukumu la kuishauri menejimenti ya chuo kuhusu masuala ya sera, mipango ya maendeleo, ubora wa mafunzo na uhusiano wa chuo na wadau wa sekta ya utalii na ukarimu.
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa taasisi za mafunzo ya utalii kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, weledi na maadili ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira na kuchangia ipasavyo katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta ya utalii, ambayo ni miongoni mwa nguzo kuu za pato la Taifa na ajira nchini.
