Arusha. Jumla ya wanafunzi 40 wa shule za sekondari zinazopatikana ndani ya eneo la hifadhi ya jamii ya wanyamapori ya Burunge, wilayani Babati, wameteuliwa kuwa mabalozi wa kuhamasisha utalii na uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wanafunzi hao kabla ya kuanza safari ya mafunzo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Ngorongoro, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara, Emmanuela Kaganda, amesema kuwa baada ya ziara hiyo, wanafunzi hao watakuwa mabalozi wa utalii na uhifadhi wa Burunge WMA, eneo lenye umuhimu mkubwa katika sekta ya utalii nchini.
Ziara ya wanafunzi hao, wakiwa pamoja na baadhi ya wazazi wao, walimu, maofisa elimu, viongozi wa serikali za vijiji na WMA, ilianza Desemba 15 na itakamilika Desemba 18,2025.
Aidha Safari hiyo imefadhiliwa na taasisi ya Chemchem Association, ambayo imewekeza katika maendeleo ya utalii wa picha na huduma za hoteli katika eneo hilo.
Kaganda amesema kuwa wanafunzi hao wanatarajiwa kuwa mabalozi wazuri wa utalii na uhifadhi katika eneo la Burunge WMA, lililoko kati ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Manyara, na lililo na umuhimu mkubwa katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
“Tunatarajia nyie mtakuwa mabalozi wa kulinda eneo hili, ambalo ni njia ya wanyamapori, ili lisivamiwe au kuharibiwa, bali lihakikishwe kuwa vizazi vijavyo litapata kuona wanyamapori salama,” amesema Kaganda.
Aidha, Kaganda amesisitiza kuwa urithi wa hifadhi za Taifa, ulioanzishwa na Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere, ni mali ya Watanzania wote na unapaswa kurithishwa kwa vizazi vijavyo.
“Naipongeza sana Chemchem Association kwa kufadhili wa safari hii ya mafunzo. Mkaone maeneo yaliyohifadhiwa vizuri, muone wanyamapori na mjifunze faida za uhifadhi mje kusaidia jamii inayowazunguka kuelimika.”
“Naagiza, watoto hawa wakirudi, uongozi wa Burunge WMA ukutane nao na kuwaeleza faida za uhifadhi, mapato yanayopatikana kila mwaka na mgao wa fedha kwa kila kijiji,” ameongeza.
Meneja Mkuu wa Chemchem Association, Clever Zulu, amesema kuwa wanafunzi hao walichaguliwa baada ya kufanya mitihani ya uhifadhi na kuonyesha utendaji mzuri.
“Tunatarajia wanafunzi hawa wawe mabalozi wa utalii na uhifadhi na wakirudi, wawe chachu ya jamii kuendeleza uhifadhi nchini. Mradi huu tulianzisha mwaka huu na tunatarajia uendelee kila mwaka ili kuzalisha mabalozi wengi wa utalii na uhifadhi.”