WAKATI usajili wa dirisha dogo unaotarajiwa kufunguliwa Januari Mosi 2026 ukikaribia, uongozi wa Mbeya City umemalizana na aliyekuwa kiungo wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana kwa kumsainisha mkataba wa mwaka mmoja.
Kulandana amejiunga na Mbeya City baada ya kuvunja mkataba wa miezi sita uliobaki katika timu ya Fountain Gate aliyoitumikia kwa msimu mmoja na nusu.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Mbeya City, kililiambia Mwanaspoti ni kweli wamenasa saini ya kiungo huyo ambaye pia alikuwa anatajwa kujiunga na Simba tangu dirisha kubwa la usajili msimu huu.
“Mambo yameenda vizuri, tumemalizana na Kulandana, kinachosubiriwa ni dirisha kufunguliwa ili kumtambulisha mchezaji huyo, tunatarajia mambo makubwa kutoka kwake kutokana na uwezo wake mzuri alionao,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Viongozi wamekamilisha kwa uharaka usajili huo kutokana na ripoti ya kocha kuhitaji mchezaji wa aina yake na ametuahidi kuipambania Mbeya City ili kufikia malengo ya kuendelea kucheza ligi msimu ujao.”
Akizungumza na Mwanaspoti, Kulandana amesema ni kweli kuna mazungumzo baina yake na timu hiyo, huku akibainisha suala la dili kukamilika taarifa itatolewa na viongozi, yeye kazi yake ni kucheza.
“Ni kweli kuna mazungumzo yanaendelea na Mbeya City, lakini bado hatujafikia makubaliano, nafikiri mambo yakienda vizuri kila mmoja atafahamu kupitia mimi au taarifa kutoka kwa viongozi wa timu hiyo,” amesema Kulandana.
