Shinyanga. Mkazi wa Mtaa wa Mwasele kata ya Kambarage mjini Shinyanga, Agness James (33) ameteketea baada ya kurudi ndani ya nyumba inayoungua kuchukua fedha zake.
Mashuhuda wa tukio lililotokea saa saba usiku wa Desemba 16, 2025 wameeleza kuwa walisikia watu wakipiga yowe na kuomba msaada, ndipo wakaelekea eneo la tukio.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 16, 2025 katika Mtaa wa Mwasele, Manispaa ya Shinyanga mume wa Agness, Vicent Kilocha amesema:
“Nilihisi kama vitu vinatembea sebuleni, nilipoamka huo usiku kwenda kuangalia nikaona moshi unatokea sebuleni, nikaenda kuwaamsha watoto pamoja na mke wangu, tukatoka wote nje, ndipo nilipoenda kuomba msaada kwa jirani.
Picha za tukio la nyumba kuteketea moto iliyopo katika mtaa wa Mwasele kata ya Kambarage Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.
Baada ya kuokoa familia yote, amesema alienda kwa majirani kuomba msaada kwa kuwagongea mageti yao kwa kuwa simu alikuwa ameacha ndani katika harakati za kuokoa familia yake.
“Niliporudi kuwauliza watoto mama yenu yuko wapi, wakasema amerudi ndani kuchukua pesa zake lakini kwa wakati huo moto ulikuwa umekuwa mkubwa zaidi nikashindwa kurudi ndani kumuokoa tena, tukawapigia Zimamoto, walifanyikiwa kuuzima lakini kila kitu kimeteketea,” amesema Kilocha
Akizungumzia tukio hilo David Johnson ambaye ni jirani, amesema: “Muda nafika moto ulikuwa mkubwa na watu walikuwa wakimuulizia mama mwenye nyumba ambaye ni marehemu, wakidai ameingia ndani. Tukapambana kuuzima kwa mchanga na maji lakini ulizidi kuongezeka.
“Basi tukawapigia Zimamoto walifika eneo la tukio na kuuzima, tulipoingia ndani tukakuta mwili wa mama huyo akiwa amepoteza maisha, polisi wamechukua mwili wake na kuondoka nao kwa uchunguzi Zaidi,” amesema Johnson.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mwasele Cosmas Lucas ameeleza kuwa, “Nilipata taarifa majira ya saa tisa usiku ndipo nilipofika eneo la tukio moto ulikuwa mkubwa sana tulipopiga Zimamoto simu ilikuwa inakatakata, tukaamua kuwafuata kwa pikipiki kuwapa taarifa,” amesema Lucas.
Ofisa Oparesheni Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Shinyanga, Edward Selemani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akitaja chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme.
Picha za tukio la nyumba kuteketea moto iliyopo katika mtaa wa Mwasele kata ya Kambarage Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.
Selemani ametoa wito kwa wananchi kuwa na desturi ya kubadilisha mfumo wa nyaya za umeme mara kwa mara, pia kuepuka kuweka vifaa vingi vya umeme kwenye chanzo kimoja.
“Taarifa tulizipata na kufika eneo la tukio ilikuwa majira ya saa tisa usiku tufanyikiwa kufika eneo la tukio na kuzima moto, baada ya kuzima tulitoa mtu mmoja ambaye ni mama mwenye nyumba akiwa tayari amepoteza maisha huku ameshikilia pesa ambazo alizirudia mkononi” amesema Ofisa Selemani.
