Dodoma. Watanzania wametakiwa kujenga utamaduni wa uwazi na uwajibikaji na kubaini makosa kabla hayajawa makubwa, pia viongozi wameelekezwa kuacha alama kwa maeneo ama taasisi wanazokabidhiwa kuziongoza.
Wito huo umetolewa leo Jumanne Desemba 16, 2025 na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IoDT) Said Kambi wakati wa kusaini mkataba wa makubaliano ya kuwajengea uwezo viongozi wa bodi za mashirika yasiyokuwa kuwa ya kiserikali.
Mkataba huo umesainiwa na Taasisi ya Wakurugenzi na Baraza la Taifa la Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NaCONGO) ambao unalenga kuwajengea uwezo katika mafunzo na kubadilishana mbinu kwa viongozi ili aweze kuzisaidia taasisi zao kuwa imara.
Kambi amesema IoDT inalenga kuelekeza namna viongozi wanavyopaswa kuongoza kwa vitendo hivyo lazima kuwa na uongozi imara wenye kuzingatia weledi na uwazi katika matumizi ya fedha, lakini akasema uwezo pekee hauwezi kusaidia kama hakutakuwa na mbinu za kisasa.
Mtendaji mkuu wa Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IoDT) Said Kambi akiingia makubaliano na Katibu mkuu wa NaCoNGO Francisca Mboya jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Amesema ni lazima taasisi ziendeshwe kitaalamu kwani wananchi wamekuwa na imani kubwa kutoka kwenye mashirika hayo, lakini itasaidia kama wataongozwa na watu wenye uadilifu na weledi mkubwa usiotiliwa shaka.
Akizunguza kwenye hafla hiyo, Mratibu wa NaCONGO Mkoa wa Dodoma, Peter Malya amesema moja ya eneo ambalo limekua na changamoto ni viongozi wa bodi za mashirika hayo, ambako amesema wakijengewa uwezo watakuwa na usimamizi imara katika taasisi zao.
Mtendaji mkuu wa Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IoDT) Said Kambi akiingia makubaliano na Katibu mkuu wa NaCoNGO Francisca Mboya jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Malya amesema bila bodi imara na mifumo mizuri kutoka kwa viongozi wa taasisi mambo mengi yatakuwa kinyume na matarajio na itakuwa ni kujidanganya, kwamba taasisi inaweza kusimama wakati hakuna wa kuisimamisha na hata aliyepo anaweza kuwa hana uwezo.
Amesema mara kadhaa baadhi ya viongozi wamekuwa na utamaduni wa kuhodhi ofisi hata wakiwa nje ya ofisi wanaondoka na nyaraka zote kiasi cha kuhisi kama taasisi ni mali yake, lakini ikitengenezwa mifumo mizuri inaweza kuwa kichocheo cha mafanikio na watu kutambua mipaka ya utendaji kazi wao.
Mchungaji John Malale amesema katika kipindi hiki ni vema kujitathimini kwa mashirika kwani nchi wahisani zinapoelekea kukata misaada yao inapasa mashirika kuwa yamejiandaa.

