Gamondi aivimbia Nigeria AFCON 2025

KOCHA wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, amesema hana hofu wala presha na safu ya ushambuliaji ya Nigeria inayoongozwa na nyota wa Galatasaray, Victor Osimhen kwa kueleza anaijenga timu hiyo kwa mfumo na mkakati unaoweza kuhimili presha ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.

Taifa Stars iliyopangwa Kundi C, itatupa karata yake ya kwanza Desemba 23 mwaka huu kwa kuikabili Nigeria, kabla ya kucheza na Uganda kisha kumalizia makundi dhidi ya Tunisia.

Kundi hilo linaloonekana kuwa gumu kwa Taifa Stars, lakini Gamondi anaamini maandalizi wanayofanya huko Misri yanatoa nafasi kwa Tanzania kushindana.

Gamondi amesema anaifahamu vizuri Nigeria, lakini hataki kikosi chake kiingie uwanjani kwa hofu ya majina.

“Nigeria ni timu kubwa, ina wachezaji wa kiwango cha juu kama Osimhen, lakini soka la kisasa halishindanishwi kwa jina. Tunajenga mfumo imara ambao utatusaidia wakati wa mashindano,” amesema Gamondi.

Kocha huyo raia wa Argentina, alieleza kuwa maandalizi ya Stars yamejikita katika kuongeza ushindani wa ndani ya kikosi, uimara wa kisaikolojia kwa wachezaji na umakini wa kimbinu.

Kwa mujibu wake, timu itacheza kwa nidhamu kubwa, kuzuia mianya kwa wapinzani na kutumia kasi kwenye maeneo ya pembeni.

Gamondi aliongeza kuwa: “Nigeria ina ubora kila idara. Hatutamwangalia Osimhen peke yake, tunajiandaa kudhibiti mfumo mzima wa Nigeria. Ukivunja muunganiko wao, unadhibiti nguvu yao.”

Kocha huyo pia alisifu mwenendo wa wachezaji wa Stars katika kambi iliyopo nchini Misri, akisema morali iko juu na ushindani wa namba umeongeza ubora wa mazoezi. Alibainisha kuwa baadhi ya wachezaji wanaocheza nje ya nchi wameongeza uzoefu na kasi ya mchezo, jambo linalosaidia kutekeleza mpango wa kiufundi.