Watu watano wakiwemo askari polisi wafariki ajalini, tisa wajeruhiwa

Watu watano wamefariki dunia wakiwemo askari wawili wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya na wengine tisa kujeruhiwa wakiwemo wanafunzi katika ajali ya barabarani iliyotokea saa 12:15 jioni ya jana Jumanne, Desemba 16, 2025.

Taarifa ya Polisi Mkoa wa Songwe iliyotolewa leo Jumatano, Desemba 17, 2025 imeeleza ajali hiyo ilitokea eneo la Karasha, Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, kwenye Barabara Kuu ya Mbeya—Tunduma.

Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Mitsubishi Canter Boxbody, mali ya Security Group of Africa (SGA) Tawi la Mbeya, lililokuwa likitokea Tunduma kwenda Mbeya likiwa na askari Polisi wawili waliokuwa wakisindikiza fedha, pamoja na pikipiki aina ya Fekon na gari aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Tunduma.

Taarifa hiyo ya Polisi imewataja waliofariki dunia ni H.7042 CPL Chirungu Misango John, WP.15582, PC Amina Japhari Hamisi.

Kutokana na ajali hiyo, watu watano (5) walifariki dunia, wakiwemo askari Polisi wawili wa Polisi Mkoa wa Mbeya, na watu tisa (9) walijeruhiwa na kupelekwa hospitalini kwa matibabu, waliofariki ni pamoja na Adam Martin (38), dereva wa Toyota Coaster, mkazi wa Mbeya, dereva wa pikipiki majina bado hayajafahamika, mwanaume mwenye umri unaokadiriwa kuwa miaka 30-35, na abiria majina bado hayajafahamika mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25-29.

Aidha, majeruhi katika ajali hiyo ni, Mariam Charles Kipangula (30), Mkazi wa Mlowo, abiria wa Coaster, Getruda Mndulo (20), Mkazi wa Chimbuya, abiria wa Coaster, MG.291715 Shukrani Nduka (40), Mlinzi SGA, mkazi wa Mbeya (ameumia mkono wa kushoto), Gadi Myegeta (46), kondakta wa Coaster, Mkazi wa Mbeya, Mariam Ramadhani (37) mkazi wa Mbeya, abiria  wa Coaster.

Orines Ngoda (14), mwanafunzi wa  kidato cha pili, Joy Girls Sekondari Tukuyu, abiria wa Coaster, Hosea   Ngoda (7) , mwanafunzi darasa la pili, Shule ya Msingi Julius, Mkazi wa Mbeya, Samwel   Mbeyela (42), dereva wa Mitsubishi Canter, mlinzi SGA na mwanamke asiyejulikana jina, umri unakadiriwa kuwa miaka 28-31.

Polisi wamesema uchunguzi wa awali umebaini  chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa gari Coaster, aliyeigonga pikipiki iliyokuwa mbele yake, kisha kupoteza uelekeo na kugongana uso kwa uso na gari Coaster, hali iliyochangiwa na mwendo kasi katika eneo la makazi ya watu.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, linatoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani, hususan kuepuka mwendo kasi, kuzingatia alama, michoro na sheria za usalama barabarani, na kuendesha kwa tahadhari katika maeneo ya makazi ya watu, huku wakitambua utii wa sheria ni msingi wa kulinda maisha ya watumiaji wote wa barabara,” imeeleza taarifa hiyo.