RAIS MWINYI: TAASISI ZA ELIMU YA JUU NI MSINGI WA MAENDELEO YA TAIFA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Taasisi za Elimu ya Juu zina mchango mkubwa katika kukuza sekta ya elimu na kuandaa rasilimali watu wenye ujuzi, maarifa na weledi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 17 Disemba 2025, alipokuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema elimu ni ufunguo muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira bora ya kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa vijana wengi zaidi, ili waweze kujijengea ujuzi, weledi, maarifa na uzalendo kwa Taifa lao.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030, imeweka mikakati na mwelekeo mahsusi wa kuhakikisha vijana wengi wanapata fursa za elimu ya juu, ikiwemo kutoa mikopo ya elimu kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya Diploma.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Vyuo Vikuu nchini katika kuandaa na kuzalisha rasilimali watu na wataalamu katika sekta mbalimbali, ikiwemo afya, elimu, sayansi na uhandisi, sekta ambazo ni nguzo muhimu za maendeleo ya kiuchumi ya Taifa.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amevitaka Vyuo Vikuu nchini kujikita zaidi katika kufanya tafiti zenye tija zitakazosaidia kutatua changamoto za kijamii na kuleta maendeleo endelevu katika nyanja mbalimbali.

Vilevile,  Rais Dkt.Mwinyi amewataka wahitimu kutumia elimu na maarifa waliyoyapata kutatua changamoto katika familia na jamii, kuishi kwa kuzingatia maadili na nidhamu, pamoja na kutimiza ndoto zao za kielimu na kimaisha.

Katika Mahafali hayo, jumla ya wahitimu 1,146 wametunukiwa Shahada mbalimbali ikiwemo Shahada ya Kwanza, Shahada ya Pili, Diploma na Vyeti, kwa mwaka wa masomo 2024/2025.