Dar es Salaam. Kilio cha msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma, mkoani Songwe, kimemsukuma Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kuagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuvunja ukuta wake ili kupanua barabara.
Mwigulu amesema hayo leo, Desemba 17, 2025, mkoani Songwe, akiwa katika ziara ya kikazi.
Ameagiza kuvunjwa kwa ukuta huo uliopo pembezoni mwa barabara ya Tunduma ili ipatikane nafasi ya kupanua barabara hiyo na kwamba ameshazungumza na Kamishna Mkuu wa TRA.
Barabara hiyo, inayojulikana kwa umuhimu wake katika kubeba uchumi wa Mkoa wa Songwe, imekuwa ikilalamikiwa mara kwa mara kutokana na msongamano wa malori yanayoingia na kutoka nchini.
“Kazi ianze mara moja, na nilishaambiwa kuna uhitaji wa kusogeza ukuta ili kupata nafasi ya kujenga barabara. Nimeshaongea na TRA na nimewaelekeza wasaidizi wake jambo la kuhamisha ukuta lianze mara moja.
“Anzeni maandalizi ya kupanua barabara ili ziweze kupita njia tatu hadi nne. Mliopewa kazi, muanze mara moja,” amesema.
Mwigulu amesema hata taasisi nyingine zilizopo karibu na eneo hilo pia ziitwe ili nafasi ipatikane, lengo likiwa ni kuondoa foleni ambayo imekuwa kero katika eneo hilo.
Agizo hilo linatokana na kilio cha ufinyu wa barabara hiyo kilichowasilishwa awali na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Makame, aliyesema msongamano wa malori unasababishwa na ufinyu wa barabara.
Awali, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, amesema yalitolewa mapendekezo barabara ya njia moja ipanuliwe ziwe njia nne.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kiini cha msongamano huo ni zaidi ya wembamba wa barabara, kwani yapo mambo mengi yanayohusishwa na hali hiyo, ikiwamo vitendo vya rushwa.
Sambamba na rushwa, wamiliki binafsi wa maegesho ya magari wametajwa kuhusika kushiriki mchezo wa kusababisha msongamano huo ili kutengeneza mazingira ya kujiingizia kipato.
Muonekane wa juu wa magari yakiwa foleni katika foleni Tunduma.Picha na Maktaba
Wapo wanaohusisha msongamano huo wa malori na mchezo mchafu unaochezwa na mawakala wa magari, wakishirikiana na wamiliki wa maegesho ili wapate kipato, kama ilivyoelezwa na Shaibu Mohamed, mmoja wa madereva.
Kwa mujibu wa Mohamed, mawakala hao hutengeneza mazingira ya kuchelewesha nyaraka za kuruhusu magari kuvuka mpakani ili mengi yalazimike kulipa tozo ya maegesho, ambayo mawakala hupata mgawo. Katika ufafanuzi wake, alisema katika Sh5,000 ya ada ya maegesho inayotozwa gari moja, wakala hupata mgawo wa Sh2,000 na mmiliki wa maegesho hubaki na Sh3,000.
“Mawakala huchelewesha nyaraka makusudi ili gari inapoegeshwa zaidi kwenye maegesho yao, wapate kiasi hicho cha Sh2,000 kwa kila Sh5,000 ya gari lililoegeshwa,” alisema Mohamed.
Lawama nyingine iliyowaangukia mawakala inatolewa na Katibu wa Taasisi ya Madereva Tanzania, Nelson Mpinzile, aliyesema dereva wa gari analazimika kutoa kati ya Sh10,000 hadi Sh20,000 ili kuruhusiwa kuvuka haraka.
“Nakupatia majina ya kampuni za mawakala wanaojifanya miungu watu kwa kusababisha foleni, hivyo bila kudhibiti utendaji wao, hata ijengwe barabara ya njia sita au nane, foleni itaendelea kuwapo,” alisema Mpinzile alipozungumza na Mwananchi.
Sababu nyingine iliyotajwa na madereva ni ucheleweshaji wa nyaraka za magari ya mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hasa yale yanayobeba mizigo ya kawaida, huku yale ya matangi yakipata nyaraka kwa wakati, kama anavyoeleza dereva Hassan Yusuph.
Kwa mtazamo wake, kuna haja na umuhimu wa mifumo ya TRA na mamlaka nyingine kusomana ili kutoa huduma kwa uwiano na kwa haraka.
Hata hivyo, Katibu wa Mawakala wa Kituo cha Forodha Tunduma, Masudi Mandimo, alikana tuhuma za mawakala kushirikiana na wamiliki wa maegesho, akisema utendaji wao unazingatia miongozo.
Alisema mawakala hawahusiki kusababisha msongamano huo, bali wanashirikiana na Jeshi la Polisi kuvusha magari, kwa kuwa kazi yao ni kutafuta wateja na kuwawakilisha mabosi wao waliopo Dar es Salaam, pamoja na kutengeneza nyaraka za magari yanayotoka Zambia na Kongo kwenda Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Mwigulu pia ametoa maagizo yatakayowaadabisha watumishi wazembe, viongozi wasiojali wananchi na wakandarasi wasio waaminifu wanaopewa miradi ambayo wanasuasua kuitekeleza.
Amesema viongozi na watumishi wazembe wasiojali wananchi watakutana na fyekeo la kufukuzwa kazi, si kusimamishwa wala kuhamishwa.
Akirejea sakata la viongozi wanane wa halmashauri za Wilaya za Mafia (Mkoa wa Pwani) na Kilolo (Mkoa wa Iringa) waliosimamishwa kazi kwa tuhuma za usimamizi dhaifu wa fedha za miradi ya maendeleo katika wilaya hizo, amesema kuwa iwapo watabainika na makosa, watatimuliwa kazi.
Watumishi waliosimamishwa ni Mkuu wa Idara ya Fedha na Ofisa Utumishi na Rasilimali Watu wa Wilaya ya Mafia, pamoja na Mkuu wa Idara ya Fedha na Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Iringa.
Hatua ya kusimamishwa kazi kwa maofisa hao ilitangazwa Desemba 14, 2025, na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Elimu, Reuben Kwagilwa, wakati wa vikao vya majumuisho ya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Kilolo na Mafia.
“Namuelekeza Katibu Mkuu Tamisemi na Utumishi hawa watu waliosimamishwa wakamilishe uchunguzi haraka. Mkijiridhisha wana makosa, wafukuzwe na wasihamishwe wala kusimamishwa. Nchi hii haina upungufu wa watu wa kufanya kazi,” ameagiza.
Amesema watumishi lazima waiogope mali ya umma, na wale viongozi wanaowapuuzia wananchi kila wanapoingia ofisini watakiona cha moto.
Kwa upande wa wakandarasi, Mwigulu amesema kitendo cha Serikali kuwaamini kutekeleza miradi ya nchi kinapaswa kuendana na utekelezaji wake.
Amesema wale wenye tabia ya kudhoofisha utekelezaji, huku wameshalipwa na baadaye kuomba kuongezewa muda, ni kuihujumu nchi, huku akiahidi kuwashughulikia.
Pia, Mwigulu ameagiza kufanyika tathmini kwa wakandarasi wa kigeni wanaotekeleza miradi nchini, huku akionesha wasiwasi kuwa wapo wasiowaaminifu wasiotekeleza miradi kwa wakati, akitaka washughulikiwe.
“Nimepita maeneo tofauti nimeona huu utaratibu ukijitokeza kwa watu kulipwa na kuahirisha mradi ambao wamepewa fedha kwa ajili yake, na kuanza kutekeleza miradi mingine na mambo mengine.
“Mkandarasi anapewa fedha kumbe anadaiwa na benki, anatumia fedha ya mradi kwenda kupooza madeni yake. Nimepita jana Mbinga nikakutana na jambo la aina hii, nikapita na sehemu nyingine nikakutana na jambo la aina hii. Nimeelekeza Tanroads, Tarura, na Naibu Waziri yuko hapa,” amesema, na kuongeza:
“Fanyeni sensa ya miradi yote ambayo wakandarasi walishapewa fedha. Muangalie fedha iliyokwishatolewa inalingana kwa kiwango gani na kazi iliyofanyika. Nipate taarifa hiyo, na wale watakaobainika kazi iko chini na fedha walizopewa, hiyo ni hujuma, lazima wafikiwe na mkono wa sheria,” amesema.
Amesema kitendo hicho kinasababisha miradi kusuasua, ambapo baadaye wanaiiongezea Serikali mzigo kwa kuomba muda wa nyongeza.
“Hawa lazima wafike kwenye mkono wa sheria. Ifuatilieni, fanyeni hiyo sensa, nataka hiyo ripoti, na nimefuatilia nimejua kuna baadhi ya wakandarasi, akiwemo mmoja ambaye mlimtoa kule Mbinga, asipate kazi nyingine yoyote hapa nchini.
“Wapatieni wazawa. Anakujaje mtu anatoka huko mnampa hela, anachezacheza hapa, anatuchezea? Wale wote ambao mnawapa kazi wanahamisha fedha, wanazitumia kwenye madeni yao, hawalipi wazawa, wasipate kazi tena. Waaminini wazawa, wapeni kazi hizo,” amesema.
Amesema na kama ni kazi, basi wapewe kazi watu wenye uchungu na nchi, huku akitaka nidhamu.
Kwa upande mwingine, amesema amani inapaswa kulindwa kwa kuwa mnufaika wa kwanza wa amani ni mwananchi mwenyewe.
“Tuache kufuata maelekezo ya watu walioko nje ya nchi kufanya vurugu, wakati tunaoumia ni sisi,” amesema.