Tanzania yajibu zuio la Marekani

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imejibu uamuzi wa Marekani kuiweka nchi katika kundi la mataifa 15 yaliyowekewa uthibiti wa visa vya kuingia nchini humo, ikisema itaendelea na mazungumzo ya kidiplomasia ili kupata muafaka unaolinda maslahi ya wananchi wa pande zote.

Kupitia taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyotolewa leo, Desemba 17, 2025, Tanzania imeeleza kuwa hatua hiyo iliyotangazwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, Desemba 16, 2025, na inahusisha pia nchi nyingine 14 za Afrika, zikiwamo Nigeria, Senegal, Zambia na Zimbabwe.

Serikali ya Marekani imeeleza kuwa udhibiti huo umetokana na taarifa ya ukaaji wa zaidi ya muda (overstay report), ikionesha baadhi ya raia wa Tanzania kuzidisha muda wa kukaa kinyume na masharti ya viza kwa viwango vya asilimia 8.30 kwa viza za B-1/B-2 na asilimia 13.97 kwa viza za F, M na J.

Hata hivyo, Serikali imesisitiza kuwa zuio hilo si kamili, na kwamba Watanzania watakaokidhi vigezo wataendelea kupewa ruhusa ya kuingia Marekani, huku ikiwahimiza wasafiri kuzingatia masharti ya viza ili kuepusha madhara binafsi na kwa taifa kwa ujumla.

Endelea kufuatilia Mwananchi.