Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania, imejibu tamko la Marekani kuhusu kuweka vikwazo kwa Watanzania kutongia nchini humo.
Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatano Desemba 17, 2025 na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhusu hatua ya Marekani kuiweka Tanzania katika kundi la nchi 15 zilizowekewa udhibiti wa visa kuingia nchini humo, imeeleza Serikali inashughulikia suala hilo.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendeleza mazungumzo ya kidiplomasia na Serikali ya Marekani ili kupata muafaka kwa masilahi ya wananchi wote,” imesema taarifa ya Serikali.
Aidha, imewahimiza Watanzania wote wanaosafiri kwenda Marekani kuzingatia kikamilifu masharti ya viza wanazopewa ili kuepuka athari binafsi na za kitaifa.
Serikali imetoa hakikisho itaendelea kutoa taarifa kadri mazungumzo na hatua zitakavyoendelea katika kutafuta suluhu ya jambo hilo.
Uamuzi wa Marekani ulitangazwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, jana Jumanne Desemba 16, 2025, na unahusisha pia nchi nyingine 14 za Afrika zikiwamo Angola, Antigua and Barbuda, Benin, Cote d’Ivoire, Dominica, Gabon, Gambia, Malawi, Mauritania, Nigeria, Senegal, Tonga, Zambia na Zimbabwe.
Kwa mujibu wa Serikali ya Marekani, udhibiti huo umetokana na ripoti ya wakaaji unaopitiliza muda (Overstay Report) unadaiwa kuwa unaonesha idadi ya raia wa Tanzania waliokwenda Marekani na kuzidisha muda wa ukaaji kinyume na masharti ya viza walizopewa.
Ripoti hiyo imeonesha Tanzania ina kiwango cha ukaaji wa zaidi ya muda cha asilimia 8.30 kwa viza za B-1/B-2 zinazohusiana na biashara na utalii, na asilimia 13.97 kwa viza za F, M na J zinazohusiana na wanafunzi, mafunzo ya ufundi na programu za kubadilishana.
Serikali ya Marekani imeeleza viwango hivyo vilizidi kiwango kinachokubalika chini ya sera zao za uhamiaji na hivyo kusababisha Tanzania kujumuishwa katika kundi la nchi zilizowekewa udhibiti huo. Hata hivyo, imefafanua udhibiti huo si kamili na kwamba Watanzania watakaokidhi vigezo na masharti ya uhamiaji wataendelea kuruhusiwa kuingia nchini humo kulingana na taratibu na tathmini zitakazotumika.
Hata hivyo, katika taarifa yake, utekelezaji wa zuio hilo, umeelezwa kuanza kutumika rasmi ifikapo Januari, 2026.
