Profesa Shemdoe aitwisha zigo Tahosa udhibiti matukio shuleni

Arusha. Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe amewaagiza wakuu wa shule za sekondari nchini kuendelea kusimamia nidhamu na kudhibiti utoro wa wanafunzi na walimu shuleni, hatua inayolenga kuinua ubora wa ufundishaji na ujifunzaji.

Ametoa maagizo hayo leo Jumatano, Desemba 17, 2025, wakati akifungua Mkutano wa 20 wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahosa) ulioanza leo jijini Arusha.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Profesa Shemdoe amesema usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji bado unaathiriwa kwa kiwango kikubwa na utoro wa walimu na wanafunzi, hali inayosababisha kukwama kwa utekelezaji wa mitalaa na ukamilishaji wa mada zilizopangwa.

“Ufundishaji unategemea uwepo wa walimu na wanafunzi. Endapo mwalimu hatakuwepo, ufundishaji utaathirika na mada zilizopangwa haziwezi kukamilika. Hali kadhalika kwa mwanafunzi anapokuwa mtoro. Simamieni nidhamu na mdhibiti utoro kwa walimu na wanafunzi shuleni,” amesema.

Waziri huyo pia amewataka wakuu wa shule kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanafunzi na kuchukua hatua madhubuti za kuzuia mimba za utotoni kwa wanafunzi, kwa kuboresha madawati ya ushauri na unasihi, kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto, pamoja na kutumia masanduku ya kupokea na kushughulikia malalamiko.

Amesisitiza utekelezaji wa maelekezo hayo kufanywa kwa kuzingatia Programu ya Shule Salama kupitia mradi wa SEQUIP.

Aidha, Profesa Shemdoe amewaelekeza wakuu wa shule na walimu wote kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wanafunzi, walimu na wazazi au walezi, ikiwemo matumizi ya lugha yenye staha na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

“Ninawaagiza kuhakikisha huduma za Serikali kwa wananchi hazigeuki kuwa bidhaa. Nafasi ya mwanafunzi kuhamia katika shule yako haiuzwi. Najua wapo wazazi au walezi watakaowashawishi kwa fedha, zawadi au vitu vingine, lakini kumbukeni hayo si maadili ya mtumishi wa umma,” amesema.

Vilevile, amehimiza matumizi ya mifumo mbalimbali ya Tehama katika utoaji na upokeaji wa huduma ili kurahisisha utendaji kazi na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa shule.

Kwa upande wake, Rais wa Tahosa, Mwalimu Denis Otieno ameiomba Serikali kuwasaidia walimu wanaofanya kazi katika maeneo ya pembezoni kwa kuwapatia vitendea kazi, zikiwamo pikipiki, ili waweze kutekeleza majukumu yao katika mazingira rafiki.

Pia ameomba Serikali kutenga fedha zinazolingana kwa shule zote, hususan katika eneo la utawala na kufanya utafiti wa bei za soko kabla ya kutenga fedha za matumizi ya mwanafunzi kwa siku, akisema viwango vya sasa havilingani na uhalisia wa soko na husababisha madeni kwa wazabuni.

Akizungumzia maelekezo hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Nanja, Saidoti Mutayuga amesema ushirikishwaji wa wazazi ni nguzo muhimu katika kuimarisha nidhamu shuleni.

“Wazazi hawana shida ukienda nao vizuri. Wakiona matokeo mazuri ya elimu na nidhamu, hutoa ushirikiano wa hali ya juu, hata kuomba vikao wao wenyewe na kuhudhuria kwa wingi,” amesema.