Moshi. Watoto wawili, Geriel Shayo (4) na Leon Shayo (2), wamefariki dunia baada ya moto kuteketeza nyumba waliyokuwa wakiishi, huku wazazi wao wakilazwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) wakipatiwa matibabu baada ya kupata mshituko kufuatia tukio hilo.
Tukio hilo limetokea leo Jumatano, Desemba 17, 2025, eneo la Katanini, Kata ya Karanga, Manispaa ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa chanzo cha moto bado kinaendelea kuchunguzwa.
“Tulipata taarifa ya tukio la moto katika nyumba ya Caesar Shayo na baada ya kupokea taarifa hiyo tulifika eneo la tukio saa 5:18 asubuhi. Tulipofika tulikuta moto umeteketeza baadhi ya mali pamoja na watoto wawili waliokuwa ndani ya nyumba hiyo. Moto huo ulianzia sebuleni,” amesema Kamanda Mkomagi.
Ameeleza kuwa, wakati tukio linatokea, dada wa kazi alikuwa amemaliza kuwapatia watoto uji na kutoka nje kwa ajili ya kusafisha vyombo, ndipo alipoona moto mkubwa ukiwa umeanza kushika paa la nyumba.
Kamanda huyo amesema alipofanya jitihada za kuingia ndani, moto ulikuwa tayari umesambaa, hivyo kuanza kupiga kelele kuomba msaada kutoka kwa wananchi.
Kamanda Mkomagi amesema wananchi walifika eneo la tukio kwa wingi na kujaribu kusaidia kuzima moto pamoja na kuokoa watoto, lakini jitihada hizo hazikufanikiwa.
Aidha, amesema wazazi wa watoto hao walipata mshituko baada ya kushuhudia tukio hilo, hivyo kupelekwa Hospitali ya KCMC kwa matibabu zaidi.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mkomagi ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mapema pindi wanapoona dalili za moto ili kuepusha madhara makubwa.
Amesema kuchelewa kutoa taarifa kumekuwa changamoto inayoongeza ukubwa wa hasara wakati wa matukio ya moto.
Shuhuda wa tukio hilo, Erick Pessa, amesema alisikia kelele za kuomba msaada na alipofika eneo la tukio alikuta moto mkubwa ukiwaka huku watoto wakiwa bado wako ndani ya nyumba.
Amesema walijaribu kuvunja milango na madirisha ili kuingia ndani, lakini moto ulikuwa mkubwa kiasi cha kushindwa kuwaokoa.
Shuhuda mwingine, Michael John amesema awali walidhani kelele walizozisikia ni za watoto wakicheza, lakini baadaye walibaini ni ishara ya dharura walikimbilia eneo la tukio kutoa msaada, japokuwa jitihada zao hazikuzaa matunda.
