Taasisi 137 yaiwezesha Nida kutwaa tuzo

Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ikitwaa Tuzo ya Ubunifu katika Utawala wa Umma 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa Zanzibar, Khamis Suleiman Mwalim amezitaka taasisi za umma wasibweteke bali waongeze bidii katika kubuni vitu vitakavyorahisisha utoaji huduma kwa wananchi.

Mwalimu amesema hayo jana Jumanne, Desemba 16, 2025 wakati wa utoaji wa Tuzo ya Ubunifu katika Utawala wa Umma kwa Mwaka 2025 jijini Dar es Salaam.

Nida imetwaa tuzo hiyo baada ya kuunganisha taasisi za Serikali na binafsi katika mfumo wa ushirikishanaji taarifa, hivyo kufikisha jumla ya taasisi 137 zilizounganishwa katika mfumo kwa ajili ya kurahisisha  utoaji huduma kwa wananchi.

Mwalimu amesema ubunifu unaofanywa na taasisi mbalimbali za umma unaangazia kutoa huduma bora kwa wananchi zinazosababisha maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

“Nawasisitiza wakuu wa taasisi za umma wote kuongeza ubunifu ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi,” amesema Mwalimu.

Mamlaka imepata tuzo kutokana na juhudi za usajili na utambuzi wa watu 26,374,903 sawa na asilimia 83.8 ya watu 31,477,938  wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Hata hivyo, Nida imezalisha na kugawa kwa wananchi namba za utambulisho wa Taifa 22,259,807 sawa na asilimia 84.4 ya watu wote waliosajiliwa, sambamba na kuzalisha vitambulisho 21,245,973 sawa na asilimia 96.1 ya namba za utambulisho zilizozalishwa.

Mkurugenzi wa Nida Zanzibar, Abdallah Mmanga amesema mamlaka inatoa shukrani kwa waandaaji wa tuzo hizo kwa kutambua mchango unaotolewa na mamlaka katika kusajili, kutambua na kuwatambulisha watu katika sekta mbalimbali ili kuwezesha kupata huduma kwa urahisi.

“Tuzo hii itachochea na kuamsha ari ya kufanya kazi kwa bidii katika kuwahudumia wananchi hasa Mamlaka inapoenda kutekeleza agizo la M Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuanza kusajili watoto wanapozaliwa,” amesema Mmanga.

Aidha, ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi pamoja na wananchi kufika katika ofisi za Nida ili waweze kusajiliwa, kutambuliwa na kutambulishwa katika fursa mbalimbali za maendeleo na ujenzi wa Taifa.