Mahakama itakavyoamua hatima shauri la kupinga Tume ya Rais leo

Dar es Salaam. Hatima ya shauri la kupinga uhalali wa Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 itajulikana leo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam itakapotoa uamuzi shauri la maombi ya kibali cha kupinga tume hiyo.

Katika uamuzi huo utakaotolewa na Jaji Hussein Mtembwa, leo Alhamisi  Desemba 18, 2025, Mahakama itajikita katika hoja mbili ambazo ndizo zilizobishaniwa wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo.

Mambo hayo ni iwapo waombaji wamekidhi vigezo cha kuwepo kwa mgogoro au hoja inayobishaniwa inayohitaji kuamuliwa.

Jambo lingine ni iwapo kibali hicho kama mahakama itakitoa, kuruhusu kufungua shauri rasmi la kupinga tume hiyo, kinaweza kutumika kama zuio kwa tume hiyo kusitisha shughuli zake mpaka shauri la kuipinga litakapoamuriwa.

Shauri hilo linatokana na vurugu na uharibifu wa miundombinu na mali za umma na watu binafsi pamoja na vifo na majeruhi, kufuatia maandamano ya Oktoba 29, 2025, katika majiji na miji mbalimbali nchini.

Kufuatia matukio hayo, Novemba 18, 2025  Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume ya kuchunguza matukio hayo, wakati na baada ya uchaguzi, inayoongozwa Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mohamed Chande na akaizindua Novemba 20, 2025,

Hata hivyo, Novemba 27, 2025, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu, Rosemary Mwakitwange na mawakili wawili, Edward Heche na Deogratius Mahinyila, walifungua shauri la maombi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wenzake.

Wajibu maombi wengine ni Jaji Mkuu mstaafu, Chande (mwenyekiti wa tume hiyo) na wajumbe, Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu

Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue; Radhia Msuya, Balozi Paul Meela na Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu (IGP), Said Mwema.

Wengine ni Balozi David Kapya, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mstaafu, Stergomena Tax na Chama cha Sheria Tanganyika (TLS).

Kwa mujibu wa waombaji, TLS kilichoundwa mwaka 1954 kwa Sheria ya Bunge,  majukumu yake ya msingi ni pamoja na kukuza utawala wa sheria, uadilifu na uwazi, kulinda na kusaidia umma kupata haki na huduma za kisheria katika masuala yote yanayohusu sheria.

Shauri hilo la maombi namba 30210 ya mwaka 2025, lilisikilizwa Desemba 12, 2025 ambapo mawakili wa waombaji, Mpale Mpoki akisaidiwa na Wakili Hekima Mwasipu waliieleza Mahakama waombaji wamekidhi vigezo vyote vitatu vya kupewa kibali hicho, vilivyowekwa na sheria.

Vigezo ni pamoja na hicho kinachobishaniwa, yaani kama kuna jambo au hoja yenye mgogoro inayohitaji uamuzi, maombi kufunguliwa ndani ya muda wa miezi sita tangu kutolewa uamuzi unaokusudiwa kupingwa na waombaji kuonesha wana masilahi katika jambo hilo lenye mgogoro.

Kuhusu kigezo cha kwanza, Wakili Mpoki alieleza kwa kuangalia kiapo na kiapo kinzani ni dhahiri kuna hoja bishaniwa kwani waombaji wametoa madai na wajibu maombi wameyapinga, huku wakitaka uthibitisho.

Pia, aliirejesha Mahakama katika kanuni ya 7(6) ya Kanuni za Uendeshaji wa Mashauri ya Mapitio ya Mahakama kuwa kibali cha kufungua shauri la mapitio ya kimahakama kinapotolewa kinatumika kama amri ya kusimamisha utekelezaji wa uamuzi unaobishaniwa.

Alisema kuruhusu kuendelea kwa jambo linalobishaniwa kunalifanya shauri husika kutokuwa na maana, huku akiirejesha mahakama kwenye uamuzi wa mashauri mbalimbali na ya nje ya nchi, kuunga mkono hoja hiyo

Jopo la mawakili wa Serikali lililoongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Narindwa Sekimanga akisaidiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Daniel Nyakia na Wakili wa  Serikali, Erigh Rumisha, kwa niaba ya AG, mwenyekiti na wajumbe wa tume hiyo walipinga maombi hayo.

Hawakuwa na ubishi katika vigezo vingine viwili kuwa waombaji isipokuwa cha kwanza, kuwepo hoja yenye mgogoro.

Wakili Rumisha alidai waombaji  wameshindwa kuthibitisha kigezo hicho muhimu akidai kiapo cha pamoja cha waombaji kimejaa mawazo, maoni na mitazamo yao na  hitimisho (la madai yao), lakini hakuna hoja za msingi.

Kuhusu maombi ya kusimamisha shughuli za tume hiyo, Wakili Rumisha alidai maombi hayo hayajaungwa mkono kwenye kiapo cha waombaji.

Pia, alidai pale ambapo kuna jambo la masilahi ya umma, basi ya umma yanasimama badala ya masilahi ya mtu mmoja.

Wakili wa TLS, Ferdinand Makore alieleza mahakama wanaunga mkono maombi hayo.

Kuhusu maombi ya kusimamisha, tume hiyo, Wakili Makore alisema Kanuni ya 7(5) ya Kanuni za Uendeshaji Mashauri ya Mapitio ya Kimahakama katika hatua ya maombi ya kibali, ina mamlaka kutoa amri ya hiyo, kulingana na mazingira.

Katika shauri hilo lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, waombaji hao wanaomba kibali kufungua shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama kuomba amri za kufuta na zuio la uamuzi wa Rais wa uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo.

Pia, wanaomba kibali hicho kitumike kama amri ya kusitisha uendeshwaji wa uchunguzi wa tume hiyo hadi shauri watakalolifungua kuipinga tume hiyo, litakapoamuliwa.

Katika shauri hilo waombaji wanapinga uhalali wa tume hiyo wakidai uundwaji na uteuzi wa wajumbe wake ulifanywa kwa nia ovu kinyume cha kanuni ya haki asili ya mtu kutokuwa hakimu wa kesi yake mwenyewe.

“Mamlaka ya uteuzi ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, chama tawala, kilichoshiriki na kushinda uchaguzi uliosababisha ghasia wakati na baada ya uchaguzi, na kwa hivyo kina masilahi katika uchaguzi huo na tume hiyo,” walidai waombaji hao.

Walidai pia mjumbe Tax ni mtuhumiwa kwani alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati ghasia za uchaguzi zilipotokea, alihusika kwa namna moja au nyingine chini ya wizara yake.

Vilevile walidai majaji wakuu wastaafu hawawezi kuchunguza kwa haki vurugu hizo kwani baadhi ya mali zilizoharibiwa ni za mahakama waliyoiongoza, na kwamba IGP mstaafu hawezi kumchunguza kwa haki, kwa kuwa, IGP aliyepo anaweza kuwa miongoni mwa watuhumiwa.

Pia, walidai Amiri Jeshi Mkuu, mamlaka ya uteuzi wa tume hiyo (Rais) katika tarehe tofautitofauti alitoa maagizo kwa Polisi na Jeshi kujiandaa kwa ghasia za wakati na baada ya uchaguzi.

Hivyo, walidai wajumbe hao hawawezi kuchunguza mamlaka ya uteuzi wao.

Vilevile  walidai uundaji wa tume hiyo umekiuka masharti ya Sheria ya Tume ya Uchunguzi, Sura 32 Marejeo 2023, kifungu cha 16.

Walidai hakuna ufafanuzi wa madhumuni yake yaliyo wazi kama kifungu hicho kinaielekeza mamlaka ya uteuzi bali  yanategemea hisia tu, kinyume na misingi ya Katiba, utawala bora na utaratibu sahihi wa haki.

Walidai maneno yaliyotumika ‘uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani’ yanapunguza na kudharau vifo, watu waliopotea, miili iliyopotea, majeraha na athari kubwa kwa umma kwa jumla.

Hoja nyingine walidai Tume hiyo si huru.

Walifafanua haikujumuisha wajumbe kutoka vyama huru vya kitaaluma kama (TLS), Chama cha Madaktari, mashirika ya kijamii, ya kidini au wadau wengine huru wasio na mgongano wa masilahi, kuepuka  upendeleo kwa mamlaka ya uteuzi.

Walidai wajumbe wote ni watumishi wa umma waliostaafu, waliokuwa na nafasi za kuteuliwa na Rais, waliokula kiapo cha siri kwa Rais, ambacho hakijafutwa wakati wa kustaafu au hadi tarehe ya uteuzi kama wajumbe wa tume inayopingwa.