ACT yasema utulivu uliopo ni wanachama kuwatii viongozi wao

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman amesema utulivu uliopo nchini ni matokeo ya utii wa wanachama wa chama hicho kwa viongozi wao. 

Mwenyekiti huyo amesema hayo jana Jumatano Desemba 17, 2025  akiwa kwenye ziara Kijiji cha Makangale, Mkoa wa Kaskazini  Pemba, ziara hiyo ina lengo kutoa shukurani kwa wazee na wananchi waliofanikisha uchaguzi wa chama hicho.

Othman amedai, kama sio busara za viongozi wa chama hicho kuzungumza na wananchi wake,  kwa yaliyofanyika kwenye uchaguzi huo uliochafuliwa amani isingepatikana.

Amedai, viongozi wa chama hicho wamejitoa kuzungumza na wananchi kwa lengo la kuinusuru Zanzibar na machafuko kila ifikapo kipindi cha uchaguzi.

“Ni dhahiri kwa yaliyofanyika hayakuwa na nia njema kwa nchi na wananchi wake, bali nusura ya Mwenyezi Mungu kupitia dua zilizoombwa maeneo mbalimbali pamoja na wananchi kusikiliza kauli za viongozi ndio usalama huu,” amesema. 

Mwenyekiti huyo, amewataka wananchi kuendelea kuwa na subira na mshikamano, wakati mazungumzo ya kutafuta haki kwa njia za amani yakiendelea, huku akikitaja kijiji hicho kama kielelezo cha maeneo yenye dhamira ya kweli ya mabadiliko visiwani Zanzibar.

Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea ubunge wa  Konde,  Mohamed Said Issa amemshukuru Othman kwa elimu ya kihistoria aliyoitoa kuhusu Zanzibar na kuahidi kuwa wataendelea kuwa mabalozi wa amani.

“Sisi tutaendelea kuwa mabalozi wazuri wa amani, subira, na mshikamano jimboni hapa,” amesisitiza Mohamed Said.

Awali, Othman alishiriki katika dua maalumu iliyoandaliwa na wananchi wa Makangale katika Msikiti wa Sheikh Ibrahim Omar, iliyoongozwa na Sheikh Hassan Masoud Hassan.