Mapito ya mradi wa mwendokasi 2025

Imepita miaka tisa  sasa tangu mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT), uanze kufanya kazi ambapo kwa mwaka huu 2025 umepitia tamu na chungu ikiwamo vituo vyake kuharibiwa kwa nyakati tofauti lakini pia kufunguliwa kwa awamu yake ya pili.

Mradi huo ambao unatekelezwa kwa awamu sita, mpaka sasa awamu mbili zimekamilika na kuanza kutoa huduma ikiwamo ya Kimara na Mbagala, huku awamu ya tatu inayohusisha barabara ya Nyerere, tayari ujenzi wake umefikia asilimia 90.

Kwa Kimara mradi huu ulianza kutoa huduma mwaka 2016, huku ule wa Mbagala ukianza Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo katika barabara ya Morogoro ulianza na  mabasi 140 licha ya kuwa ulipaswa kuanza na mabasi 305. Japokuwa baadaye kuliongezwa mabasi mengine 70, ambayo yanadaiwa yaliagizwa bila kufuata utaratibu na mwendeshaji wa mradi kipindi cha utawala wa Hayati John Magufuli, hivyo kushikiliwa.

Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia uliamua kuyaingiza barabarani ili kupunguza tatizo la uhaba wa mabasi hayo barabarani.

Aidha tangu mradi huo uanze umepunguza muda wa watu kufika katika maeneo yao ya kazi na biashara, lakini pia kupunguza foleni ya magari barabarani hata hivyo ulikuwa na nyakati zake za shubiri.

Miaka ilivyozidi kwenda, kulikuwapo na baadhi ya changamoto ikiwamo uhaba wa mabasi, abiria kukaa muda mrefu vituoni bila kupata huduma.

Pamoja na hatua hiyo, kuchakaa kwa mabasi hayo kulikochangiwa kubeba abiri wengi kupita uwezo wake, kutokarabatiwa kwa wakati, kulifanya mabasi hayo kuharibika kadri siku zilivyozidi kwenda.

Katika kipindi cha mwaka 2025, mara kadhaa wananchi walikuwa wakipaza sauti zao kutaka kupatikana kwa mshindani mwingine wa kutoa huduma ukiacha Kampuni ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart).

Oktoba 2, 2025 ilisambaa video ya mitandaoni zikionyesha abiria waliojazana kwenye usafiri huo, wakipaza sauti hawataki Chama cha Mapinduzi (CCM). Video hiyo ilibua hisia za watu wengi na Serikali ikakiri kupokea kilio hicho.

Baada ya muda likitoa tukio lingine la  fujo na kuharibu miundombinu ya mradi huo kwa kupasua vioo kwa baadhi ya vituo vya mabasi hayo ikiwamo kile cha  Mwembe Chai na Magomeni Usalama.

Katika matukio hayo, Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alithibitisha watu watatu kushikiliwa wakidaiwa kuhusika na uharibifu wa miundombinu hiyo.

Hata hivyo hali hiyo ilimfanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila  kufanya ziara kituo cha mabasi  hayo Kimara, ambapo akiwa huko aliwataka wananchi kuwa watulivu  wakati Serikali ikiendelea kushughulikia changamoto ya usafiri  huo , hususan katika kituo hicho.

“Ndani ya wiki hii mabasi hayo yataanza kutoa huduma. Tayari yapo ‘yard’ yakisubiri kuingizwa barabarani. Tumekutana na kampuni husika na baadhi yataanza kazi muda wowote kuanzia sasa,” alisema Chalamila.

Ukiacha karaha hizo ilizopitia mradi huo, pia kuna hatua za mafanikio imepata, ambapo kwa mwaka huu, mradi wa awamu ya pili  unaohusisha barabara ya Mbagala hadi Kariakoo Gerezani, ulianza kazi rasmi.

Barabara hiyo ya Mbagala yenye urefu wa kilomita 20.3 kutoka Mbagala hadi Gerezani, iliyojengwa na Kampuni ya Sinohydro kutoka China na ilikabidhiwa kwa Dart tangu Agosti 2023.

Katika awamu hiyo, kampuni ya kizalendo ya Mofat ndiyo imepewa mkataba wa miaka 12 kutoa huduma hiyo na mabasi yake yatatumia nishati ya gesi asilia na yalianza kuingizwa nchini kuanzia Agosti 3,2025 .

Hata hivyo mradi huo wa awamu ya pili wote unahitajika kuwa na mabasi 755, huku Mofat peke yao akitakiwa kuleta mabasi 250. 

Hatua hiyo imekuja  baada ya danadana za muda mrefu za kuanza kwake kazi  na sasa wakazi wa maeneo hayo na yale ya jirani wameshasahau adha ya kupandia daladala  madirishani.

Lakini pia hii imesaidia kuinusuru miundombinu yake , ambayo tayari baadhi ya maeneo ilikuwa imeshaanza kuharibika kutokana na kutotumika ikiwemo taa za kuongozea magari, na vituo vyake kuharibika.

Ufanyaji kazi wake  kama majaribio ulianza rasmi Oktoba 12 ambapo mabasi hayo yakiwa tofauti na yale ya mradi wa awamu ya  kwanza unaohusisha barabara ya Kimara, yana full AC, huku kwa mujibu wa kampuni ya Mofat iliyopewa zabuni ya kuuendesha  ikieleza watakuwa na uwezo wa kusafirisha.

Hata hivyo yakiwa yamefikisha siku 17 tangu yaanze kutoa huduma, ilisitishwa kutokana na vurugu za Oktoba 29 na kurejea tena Novemba 20, 2025 ambapo mpaka sasa mbali na Mbagala hadi Kariakoo, pia yanafanya safari zake hadi Ilala Boma.

Kwa upande wa Kimara wao waliongezewa mabasi kutoka yale 30 yaliyokuwa yamesalia na kufika  90,  hii ni baada ya serikali kuyakodi mabasi 60  kwa muda kutoka kampuni ya Mafat.

Hali hii imesaidia kwa kiasi kikubwa watu kutokaa muda mrefu kituoni kusubiri usafiri huo kutokana na kila wakati kufika, lakini pia kupunguza misongamano iliyokuwa awali katika vituo vya mabasi hayo hususani Kimara, Msimbazi na Gerezani.

Maamuzi ya kuongeza mabasi hayo yalitangazwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Oktoba 2, 2025 alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma ya usafiri wa mabasi hayo Kivukoni hadi Kimara jijini Dar es Salaam.

Majaliwa alisema kuwa Serikali imeamua kuingiza mabasi 60 mapya kwenye Barabara hiyo  iliyokuwa na mabasi 30 yanayofanya kazi ili kukabiliana na upungufu wa magari uliokuwepo na hivyo kusaidia kuondoa kero ya usafiri iliyokuwepo.

“Serikali yenu baada ya kuruhusu makampuni binafsi tumeona tuchukue mabasi 60 kutoka kampuni ya Mofat yaingie katika barabara hii na yameanza kutoa huduma leo, malengo yetu ni kuondoa kadhia ya usafiri kwenye njia hii,” alisema.

Katikati ya changamoto za utoaji huduma za usafiri huo, kumekuwapo pia na changamoto ilizopitia kwa mwaka huu Ukiacha tukio la watu kurushia mawe vituo vya mabasi hayo, pia Oktoba 29 wakati wa vurugu za maandamano zilipotokea, vituo vingi vya mabasi hayo vilichomwa moto.

Novemba 25, alipokutana na waandishi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, hasara iliyotokea katika vurugu hizo, Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba alisema vituo vya mabasi ya mwendokasi 27 na mabasi sita yalichomwa moto.

Kutokana na hali hiyo, huduma za mabasi hayo zilisitishwa katika barabara zote ambapo kwa barabara ya Mbagala zilianza kurejea tena kuanzia Novemba 20, na ilipofika Novemba 29 barabara ya Kimara zilianza kutoa huduma  kutoka Kituo cha Ubungo Maji hadi Kivukoni na Gerezani, na ilipofika  Desemba 3, zilirejea  kama kawaida kutoka Kituo Kikuu cha Kimara kwenda Gerezani na Kivukoni.

Aidha watendaji nao waliokuwa wakisimamia mradi huo kwa mwaka huu hawakuachwa salama kwani  walijikuta wakitumbuliwa ndani ya mwaka huu.

Katika taarifa ya uteuzi huo iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka, Oktoba 2, 2025, ilieleza kuwa Said Tunda ameteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).

Tunda alichukua nafasi ya Dk Athumani Kihamia ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Aidha, Rais Samia amemteua Pius Ng’ingo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), akichukua nafasi ya Waziri Kindamba ambaye uteuzi wake pia umetenguliwa. Pia katika mabadiliko hayo, Rais Samia pia aliwateua Wenyeviti wapya wa bodi, ambapo Balozi Ramadhani  Dau, aliteuliwa  kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Udart huku David akiteuliwa  kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).

Hata hivyo siku chache baada ya kuteuliwa, Dau alisema aliamua kupanda kwa siri usafiri huo ili kubaini changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi na kukiri kwamba zipo na kuahidi wangejadiliana kwenye vikao vyao ili kuondoa kero hizo.

Pia Mwenyekiti huyo, ambaye aliandika andiko refu baada ya safari yake hiyo, aliwakumbusha Wakurugenzi wenzake na menejimenti kwa ujumla  kuwa dhamana waliyopewa ni kubwa na matarajio ya wananchi ni makubwa.

“Nina imani tukifanya kazi kwa juhudi, maarifa ikiwamo ubunifu na kuweka uzalendo mbele, tutatoa mchango mkubwa kwa nchi yetu,” aliandika Dau.

Wakizungumzia mradi huo, baadhi ya watumiaji wa mabasi hayo, Asteria Kimolo, mkazi wa Kimara, amesema kipindi cha shubiri  walishauona mradi huo kuwa hauna maana kutokana na mateso waliokuwa wanayapitia. Hata hivyo amesema baada ya serikali kuingilia kati na kukodisha mabasi ya Mofat walau ahueni wanaiona.

Hendry Lema, mkazi wa Mbezi, anasema ili mradi huo uweze kukidhi haja kwa watumiaji ni vema magari yakaongezwa na kufikia idadi inayoendana na mahitaji halisi.

“Tunaweza kusema ndiyo kuna afueni baada ya kuongezwa hizo gari 60, lakini ukweli ni kwamba bado kunahitajika magari mengi zaidi, kwa kuwa adha ya kubanana kwenye magari hayo bado ipo hasa nyakati za jioni na asubuhi,” amesema.

Kuruthumu Mngazija, mkazi wa Mbagala, amesema kuanza kwa mradi huo barabara ya kwenda huko kumeifanya Mbagala kupanda thamani tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

“Hii yote ni kwa sababu tu ana uhakika wa usafiri wa kwenda kwenye shughuli zake na kurudi, kwa kweli katika hili niipongeze serikali, imejitahidi japo tulikuwa tukitamani ungeanza mapema,” amesema.

Humphrey Clement, amesema ni wakati sasa wa magari madogo ya kuwapeleka abiria katika njia kuu kuanza kazi na kama shida ni miundombinu irekebishwe haraka kwa kuwa wengi wa wananchi wanatoka maeneo ya pembezoni.

“Hizi gari sawa zimeturahisia usafiri wa kwenda mjini, lakini bado wengi wetu tukishuka mwisho wa vituo, inatubidi tena kuchukua bajaji, bodaboda au daladala na hivyo kuongeza gharama katika usafiri, hivyo serikali iharakishe kuleta na zile gari za kutoa abiria maeneo ya ndanindani,” amesema Clement.

Sabrina Juma  mkazi wa Tabata yeye anasema anasubiri kwa hamu kuiona huduma ya mwendokasi katika njia ya Mandela akisema hapo sasa Dar es Salaam itakuwa imeunganishwa.