SOKO LA KARIAKOO MBIONI KUFUNGULIWA

Shirika la Masoko ya Kariakoo limekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wa soko la Kariakoo kwa lengo la kuwasikiliza na kuwapa mrejesho wa namna shirika hilo lilivyoshugulikia maoni na changamoto za wafanyabiashara ikiwa ni maandalizi ya kufungua soko hilo Januari, 2026.

Akiongea na wafanyabiashara hao, Meneja Mkuu wa shirika hilo CPA. Ashraph Abdulkarim amesema shirika hilo limefanikiwa kuwapangia maeneo wafanyabiashara wa zamani 1520 waliokidhi vigezo vya kurejea sokoni hapo na kupata wateja wapya 351 ambao wameomba kupitia mfumo wa TAUSI.

CPA. Abdulkarim ameongeza kuwa kufuatia maoni yao, mkandarasi anafanya marekebisho madogo madogo ambayo yatakamilika mapema iwezekanavyo ili soko hilo liweze kuanza kufanya kazi na kuwafanya wafanyabiashara hao kufanya biashara zao katika mazingira salama na ya uhakika.

CPA.Adbdulkarim amebainisha kuwa miongoni mwa shughuli zilizofanyika ni pamoja na kushughulikia malalamiko ya wafanyabiashara hao, kusaini mikataba pamoja na kuingiza mikataba hiyo katika mfumo wa TAUSI.

Ameongeza kuwa shirika hilo litaendelea kusikiliza na kushauriana na wafanyabiashara hao mara kwa mara kwa kutambua kuwa soko la Kariakoo ni mali yao na wafanyakazi wa shirika hilo wanafanya kazi ya usimamizi kwa niaba ya wananchi ikiwemo wafanyabiashara hao.

Serikali imekarabati na kujenga soko la Kariakoo kwa takribani Bilioni 28 na kuweka mifumo ya kisasa ya Tehama, usalama, maegesho ya magari pamoja na huduma zingine za kijamii ambayo yanaakisi mifumo masoko ya kisasa duniani.