Haya ndio matarajio mkutano wa kimataifa wa tiba asilia

Dar es Salaam. Mkutano wa pili wa Kimataifa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu tiba asilia, unaoandaliwa kwa ushirikiano na Serikali ya India, unatarajiwa kutangaza mipango ya kisayansi na ahadi mpya zinazolenga kuharakisha utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa wa WHO wa Tiba Asilia wa mwaka 2025–2034.

Mkakati huo unazingatia kuimarisha ushahidi wa kisayansi, kuboresha mifumo ya udhibiti, kuunganisha tiba asilia katika mifumo ya afya, kuimarisha ushirikiano na kuongeza ushiriki wa jamii.

Mkutano huo umefunguliwa jana Jumatano, Desemba 17, 2025 ukiwakutanisha mawaziri wa serikali, wanasayansi, viongozi wa jamii za asili, na watendaji wa tiba kutoka zaidi ya nchi 100 duniani.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa.

Mchengerwa amepongeza juhudi zinazofanywa na WHO za kuileta dunia pamoja ili kujadili suala la tiba asili na kupata ufumbuzi katika masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na utawala na udhibiti wa tiba asili, utafiti na ushahidi wa kisayansi, ujumuishaji wa tiba asili katika mifumo ya afya, matumizi endelevu  ya rasilimali za kiasili na uendelezaji wa rasilimali watu kwenye eneo la tiba asili.

Pembezoni mwa mkutano huo, Tanzania inatarajia kusaini hati mbili za makubaliano (MoU) na Serikali ya India kuhusu ushirikiano katika sekta ya afya na tiba asilia (Ayurveda), hatua itakayosaidia kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi, kuongeza uwezo wa rasilimali watu na kuimarisha matumizi salama ya tiba asilia nchini.

Kusainiwa kwa hati hizo mbili za makubaliano ni hatua muhimu kwa Tanzania, kwani kutaimarisha ushirikiano wa kitaasisi na India katika maeneo ya kipaumbele ya sekta ya afya, kuongeza uwezo wa rasilimali watu wa sekta ya afya, kuimarisha udhibiti na matumizi salama ya tiba asilia, pamoja na kuchangia jitihada za Serikali katika kuimarisha mifumo ya huduma za afya na kufikia mpango wa bima ya afya kwa wote.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unaakisi dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kukuza tiba asilia salama, yenye ushahidi wa kisayansi na inayosimamiwa kwa misingi madhubuti ya udhibiti, sambamba na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu ya afya kwa watu wote.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na WHO, mkutano huo ulianza (Desemba 17–19) 2025, New Delhi) na utatangaza ahadi mpya kutoka kwa Serikali na wadau wengine.

Pia, utatoa wito wa kuanzishwa kwa muungano wa kimataifa utakaoshughulikia mapungufu ya kimfumo na kuharakisha utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa wa Tiba Asilia kwa kiwango kikubwa.

WHO imesema, tiba asilia bado ndiyo chanzo kikuu cha huduma za afya ikiwa inapatikana kwa urahisi katika jamii, gharama nafuu na huendana na utamaduni na mazingira ya kibiolojia.

WHO inaeleza, tiba asilia ni chaguo linalopendelewa na takribani asilimia 90 ya nchi wanachama wa shirika hilo (170 kati ya 194) zinaripoti kuwa kati ya asilimia 40 hadi 90 ya wananchi wao hutumia tiba asilia.

“WHO imejizatiti kuunganisha hekima na nguvu ya sayansi na teknolojia za kisasa ili kutimiza dira ya afya kwa wote,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus.

Dk Ghebreyesus amesema kutumia ubunifu kuanzia Akili Unde (AI) hadi jenomiki (uchunguzi wa vinasaba), wanaweza kuifanya tiba asilia kutoa suluhisho la afya bora zaidi na endelevu kwa kila jamii na kwa sayari yetu.

Shirika hilo limesema, katika dunia inayokabiliwa na changamoto zinazoongezeka katika mifumo ya afya, takribani watu bilioni 4.6 hawana huduma muhimu za afya, huku robo ya idadi ya watu bilioni 2 wakikabiliwa na mzigo wa fedha wanapojaribu kupata huduma za afya.

“Kuunganisha tiba asilia katika mifumo ya afya ni jambo muhimu ili kupanua upatikanaji na chaguo la huduma za afya zilizo nafuu na zinazomlenga mtu, pamoja na kuendeleza Afya kwa Wote (UHC), kuhakikisha kila mtu anapata huduma za afya anazohitaji bila kuathiriwa kifedha,” amesema.

Msisitizo wa WHO unaeleza ushahidi unaojitokeza unaonyesha kuunganisha tiba asilia katika mifumo ya afya kunaweza kuleta ufanisi wa gharama na kuboresha matokeo ya afya.

Ujumuishaji huo unasisitiza zaidi kinga na uhamasishaji wa afya, na hivyo kuchangia manufaa mapana ya kiafya kama vile matumizi sahihi zaidi ya antibiotiki.

Mwanasayansi Mkuu wa WHO, Dk Sylvie Briand, amesema:“Tunahitaji umakini uleule wa kisayansi katika tathmini na uthibitishaji wa tiba ya kisasa na tiba asilia, huku tukiheshimu bioanuwai, upekee wa kitamaduni na kanuni za kimaadili.”

Mwanasayansi  huyo amesema  ushirikiano imara zaidi na matumizi ya teknolojia za mbele kama Akili Unde jenomiki, baiolojia ya mifumo, sayansi ya neva na uchambuzi wa hali ya juu wa takwimu vinaweza kubadilisha namna wanavyochunguza na kutumia tiba asilia.

WHO inaamini tiba asilia ni msingi wa sekta za kimataifa zinazokua kwa kasi, kama tasnia ya dawa za mitishamba.

“Mchanganyiko wote wa tiba asilia, pamoja na zaidi ya nusu ya dawa za kisasa za kitabibu, zinatokana na rasilimali za asili, ambazo zinaendelea kuwa chanzo muhimu cha ugunduzi wa dawa mpya.

“Jamii za watu wa asili hulinda takribani asilimia 40 ya bioanuwai ya dunia ilhali zinawakilisha asilimia 6 pekee ya idadi ya watu duniani. Kuendeleza tiba asilia kunahitaji kushughulikia masuala ya haki za watu wa asili, biashara ya haki, na mgawanyo wa manufaa,” taarifa ya WHO imeeleza.

Licha ya matumizi makubwa ya tiba asilia na jukumu lake muhimu katika kulinda rasilimali za asili uwekezaji wa tafiti za afya kwa kutumia tiba asilia ni chini ya asilimia moja pekee.

Ili kusaidia kuziba pengo la maarifa na utafiti, WHO inazindua Maktaba ya Kimataifa ya Tiba Asilia ya kwanza ya aina yake, yenye zaidi ya rekodi za kisayansi milioni 1.6 zinazojumuisha tafiti, sera, kanuni na makusanyo ya mada mbalimbali kuhusu matumizi tofauti ya tiba asilia.

Maktaba hiyo imeanzishwa kufuatia wito wa wakuu wa nchi wakati wa mikutano ya G20 na BRICS mwaka 2023.

Pia hutoa upatikanaji wa haki wa maudhui yaliyopitiwa na wataalamu kwa taasisi katika nchi zenye kipato cha chini kupitia mpango wa Research4Life.

Aidha, inasaidia nchi kuandika na kuhifadhi maarifa ya tiba asilia kwa ulinzi wa haki miliki na kujenga uwezo wa kisayansi ili kuchochea ubunifu.

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Tiba Asilia cha WHO, Dk Shyama Kuruvilla amesema kuendeleza tiba asilia ni hitaji la msingi linalotegemea ushahidi wa kisayansi, maadili na ulinzi wa mazingira

Amesema mkutano huo wa kimataifa unaweka mazingira na ushirikiano unaohitajika ili tiba asilia ichangie kwa kiwango kikubwa ustawi wa watu wote na sayari.