Mapato ya utalii yaongezeka kwa asilimia sita Serengeti

Serengeti. Hali ya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imezidi kuimarika, huku mapato yake yakiongezeka kwa asilimia sita katika kipindi cha Oktoba mosi 2025 hadi Desemba 14, 2025.

Mapato hayo ya utalii yamefikia Sh49.2 bilioni ikilinganishwa na Sh46.4 bilioni zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Desemba 18, 2025, na Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Fabian Manyonyi, alipozungumza na waandishi wa habari kwenye lango kuu la Naabi kuhusu hali ya utalii katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

Amesema hali ya utalii imeendelea kuimarika hifadhini humo, ikilinganishwa na kipindi cha Oktoba mosi hadi Desemba 14, 2024, ambapo watalii wameendelea kuongezeka.

Manyonyi amesema takwimu za mwaka 2023/24 zinaonyesha Serengeti ilipokea wageni 430,219 huku mapato yakiwa Sh210.9 bilioni, wakati mwaka 2024/25 watalii walikuwa 491,398 na mapato kufikia zaidi ya Sh266.8 bilioni.

“Hali yetu kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 14 mwaka huu imeendelea kuimarika, na wageni wameendelea kufanya utalii ikilinganishwa na mwaka jana katika kipindi hicho.

“Tunaendelea kuhamasisha Watanzania pia waongezeke kufanya utalii wa ndani. Ukiangalia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeendelea kutambulika kimataifa; kwa mwaka huu tumepata tuzo mbalimbali, ikiwamo ya hifadhi bora Afrika. Tuzo hizi zinaendelea kufanya hifadhi yetu ivutie watalii zaidi kuja kuitembelea,” amesema mhifadhi huyo.

Mmoja wa watalii kutoka Ujerumani, Michael Schlittenberver, amesema watakuwepo nchini kwa siku 16, wakitembelea vivutio mbalimbali ikiwamo hifadhi za taifa na Zanzibar.

Baadhi ya watalii kutoka nchi  mbalimbali, wakiwa katika mapumziko nje ya lango kuu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

“Kwa siku hizi ambazo tumeendelea kujionea vivutio na mandhari nzuri ya Tanzania, tutaendelea kuwepo hapa kwa siku hizo 16. Tutatembelea hifadhi nyingine pia. Kiukweli tumevutiwa sana na tumejionea wanyama wa aina mbalimbali pamoja na ukarimu wa Watanzania,” amesema Schlittenberver.

Naye Talvinaer Virdee, mtalii kutoka Uingereza, amesema wamejionea wanyama wengi na upekee wa Tanzania, na kwamba licha ya kuzaliwa Dar es Salaam, walihamia Uingereza akiwa na umri wa miaka sita, bado anavutiwa kuja kutembelea vivutio vilivyopo nchini.

“Nilipokuwa na miaka sita, wazazi wangu walihamia Uingereza na ninaishi huko hadi sasa. Nimekuja kutembelea ndugu zangu pamoja na kutembelea hifadhi zetu,” amesema na kuongeza;

“Nimekuja na binti yangu mmoja, ila nina wengine wawili ambao hawakuweza kusafiri, lakini nitawaleta. Ninaamini watafurahia sana. Pia nitaleta dada zangu wawili waje kujionea wanyama na mandhari nzuri ya Tanzania,” amesema.

Mmoja wa waongoza watalii kutoka Kampuni ya Wild Serengeti Quest, Fidelis Fabian, amesema katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka wameendelea kupata wageni kutoka nje wanaotembelea vivutio mbalimbali, wengi wao wakiwa wameambatana na familia zao.

“Kwa mfano, katika kampuni yetu, tumejaza nafasi katika kipindi chote. Wageni wanazidi kuongezeka na wanaamini kuna usalama, ndiyo maana wanakuja,” amesema.